Solskjaer: Tutapindua matokeo Hispania

Muktasari:

  • Bao la kujifunga la beki wa kushoto Luke Shaw limeiweka njia panda Manchester  United katika mchezo wake wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki ijayo dhidi ya Barcelona

London, England. Ole Gunnar Solskjaer atalazimika kufanya kazi ya ziada kupata matokeo mazuri katika mchezo ujao wa obo fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati  Manchester United itakapokuwa ugenini kuivaa Barcelona kwenye Uwanja wa Nou Camp.

Kipigo cha bao 1-0 ilichopata jana usiku kinamuweka kocha huyo katika nafasi ndogo ya kusonga mbele ingawa amedai ana timu imara inayoweza kufanya maajabu katika mchezo huo wa wiki ijao.

Solskjaer alisema Man United ina nafasi ya kufunga bao katika mchezo huo kwa kuwa ana kikosi imara

Mshambuliaji huyo wa zamani wa timu hiyo ana amini kama aliweza kupindua matokeo katika mchezo dhidi ya Paris Saint  Germain PSG hakuna ana nafasi pia ya kufanya hivyo Hispania.

Man United ilichapwa mabao 2-0 na PSG kwenye Uwanja wa Old Trafford kabla ya kuiduwaza dunia kwa ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya marudiano mjini Paris, Ufaransa.

“Tumepata mafanikio makubw akutokana na historia ya Barcelona. Bado tuko katika ushindani, itakuwa mechi ngumu lakini tuliwahi kufanya hivyo hapo nyuma,” alisema nguli huyo wa Norway.

Beki wa kushoto Luke  Shaw alijifunga dakika ya 12 kutokana na mpira wa kichwa uliopigwa na Luiz Suarez aliyeunganisha krosi ya Lionel Messi.

Kocha huyo aliyejaza nafasi ya Mreno Jose Mourinho, alidai timu yake haikuanza mchezo vizuri lakini baada ya Shaw kujifunga, utulivu ulirejea na timu ilitengeneza nafasi kadhaa.

“Kimsingi lilikuwa bao bora kutokana na kazi nzuri ya Messi na Suarez. Messi ni mchezaji wa aina yake,” alisema Solskajaer.

Kiungo kinda Scott McTominay alikuwa nyota wa mchezo baada ya kucheza kwa kiwango bora.

Kocha wa Barcelona Ernesto Valverde alisema mechi ilikuwa ngumu na haikuwa kazi nyepesi kupata ushindi. Alisema anakwenda kujiandaa vyema kwa mchezo wa marudiano huku akiwa na kumbukumbu ya Man United kuing’oa PSG.

Katika mechi nyingine Ajax Amsterdam ikiwa nyumbani Uholanzi ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Juventus.