Simba yawapa Yanga angalizo vurugu za mashabiki

UONGOZI wa Klabu ya Simba umezungumza na uongozi wa Yanga ili kukumbushana kuhusu wajibu wa viongozi wa klabu za soka kudhibiti vitendo vya mashabiki wao wawapo uwanjani.

Simba kupitia Mtendaji Mkuu wao, Barbara Gonzalez imesikitishwa na kukemea vikali kitendo cha baadhi ya mashabiki wa Yanga kuwapiga mashabiki wa Simba waliohudhuria mchezo kati ya Yanga na Mtibwa uliofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini  Morogoro, Septemba 27 mwaka huu.

Barbara ametoa taarifa hiyo leo Jumanne Septemba 29, 2020 kwenda kwa mashabiki na vyombo vya habari, kuwa matukio ya mashabiki wa Simba kupigwa, kuchaniwa jezi na kudhalilishwa na baadhi ya mashabiki wa Yanga yamekuwa yakijirudia siku hadi siku tena kwa kipindi kifupi.

"Hii ni ishara kwamba bila hatua kali, madhubuti  na za haraka zinazochukuliwa zaidi ya kutoa taarifa kwa umma kuelezea masikitiko tabia hizi zitaota mizizi na kuonekana ni mambo ya kawaida katika mpira.

"Tabia hizi hazipaswi kuvumiliwa kwa kuwa zinahatarisha umoja, amani na utulivu katika nchi yetu na zinajenga sifa mbaya duniani kwa soka letu", ilieleza taarifa hiyo

Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa kwa kuzingatia hayo wamechukua hatua zifuatazo

"Nimeongea na Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Wakili Patrick Simon kumueleza masikitiko yetu kuhusu matukio hayo, tumekuwa na mazungumzo mazuri ambapo nimemkumbusha kuhusu wajibu wa viongozi wa klabu kudhibiti vitendo  vya mashabiki wao wawapo mpirani  kote duniani na katika kanuni mbalimbali za TFF, CAF, FIFA na hata kanuni za uendeshaji wa ligi yetu  klabu zimepewa wajibu huo

"Pia klabu zinaposhindwa kutimiza wajibu huo ipo mifano mingi duniani ya hatua stahiki zinazochukuliwa dhidi ya klabu husika, nina imani kwamba wenzetu Yanga kwa kuzingatia kwamba matukio haya yanajirudia watachukua hatua muafaka.

"Tumeandika barua rasmi TFF kuelezea masikitiko yetu na kupendekeza hatua za kuchukua. Vyombo vya Ulinzi na Usalama vina nafasi yake pia TFF na Bodi ya Ligi nazo zina nafasi yao na zina wajibu wa kuchukua hatua na hazipaswi kukwepa wajibu huo, tunatarajia kwamba hatua zitachukuliwa haraka," imeeleza.

Barbara amewataka mashabiki wa Simba kutulia wakati uongozi unatumia njia na mamlaka rasmi ili kulinda hadhi na heshima ya klabu hiyo na soka la Tanzania na kulinda utu wa mashabiki wao.

"Tunawaomba mashabiki wetu wasichukue hatua zozote za kulipa kisasi wala wasifanye fujo ya aina yoyote dhidi ya mtu yoyote, Uongozi kama ilivyo kwa Watanzania wote tuna wajibu wa ulinzi na amani na utulivu wa nchi yetu, umoja, upendo  na mashikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania.Tusingependa kabisa ushabiki wa soka awe chanzo cha chuki, mifarakano na uvunjifu wa amani katika jamii.

"Simba itaendelea kuwa klabu ya mfano kwa ubora wa mpira wetu, ndani ya uwanja na nidhamu na ustaarabu  wa washabiki wetu nje ya uwanja" imeeleza taarifa hiyo iliyoandikwa na Barbara.