Simba yaionyeshea umwamba Ruvu Shooting

Muktasari:

Hilo linakuwa bao la tano kwa Miraji Adam tangu Ligi Kuu Bara ianze msimu huu.

BAO la dakika ya 39 lililofungwa na Miraji Adam limeipeleka Simba mapumziko dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Miraji alifunga bao hilo kwa kichwa akimalizia krosi ya Shomari Kapombe ambaye nae alipokea pasi nzuri kutoka katikati ya uwanja iliyopigwa na Hassan Dilunga. Bao hilo linakuwa la tano tangu kuanza kwa ligi giyo msimu huu.
Mchezo huo ulianza kwa kasi lakini Simba ndio walionekana wana mipango zaidi  ya kutafuta bao la mapema kwani dakika 20 za mwanzo walifanya mashambulizi mengi  kuliko wapinzani wao Ruvu Shooting.
Dakika ya tatu Simba ilifanya shambulizi zuri langoni kwa Ruvu Shooting lakini beki  Pascal Wawa alishindwa kumalizia pasi ya Francis Kahata na kupiga shuti lililotoka nje ya lango.
Simba iliendelea kutafuta bao kwa nguvu na dakika ya saba Mzamiru Yassin aliachia shuti kali nje kidogo ya 18 lakini likadakwa vema na kipa wa Ruvu Shooting, Mohammed Makaka.
Dakika ya 16 mshambuliaji wa Ruvu Shooting, Sadat Mohammed aliambaa na mpira na kuachia shuti lililopanguliwa na kipa Aishi Manula kabla ya beki Mbrazil Tairone Santos  kuuwahi mpira huo na kuuokoa.
Simba iliendelea kulisakama lango la Ruvu Shooting kama nyuki na  dakika ya 23 nusura Dilunga aifungie timu yake bao kama si juhudi za kipa wa Ruvu, Makaka kupangua mpira na kuwa kona tasa.
Hata hivyo safu ya ulinzi ya Ruvu inayoongoza na Rajab Zahir, Renatus Ambrose na Omary Kindamba  inastahili sifa kwa kuwadhibiti Simba hasa kupitia mipira ya juu waliyokuwa wakipiga kupitia kona au krosi na mabeki hao kuokoa mara kwa mara.