Simba na Yanga ni leo Dar

LEO Ijumaa katika Uwanja wa Simba Mo Arena utapigwa mtanange wa Ligi Kuu ya Wanawake kati ya Simba Queens na Yanga Princess huku makocha wakijitapa.

Simba Queens endapo watashinda pambano hilo watabaki kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakiwa na alama 38, huku Yanga wakipata pointi tatu watabaki katika nafasi ya tano na alama 26.

Huo utakuwa ni mchezo wa nne timu hizo kukutana kwenye mashindano hayo huku Simba wakiwa wababe zaidi na Yanga wakiendelea kuchechemea. Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilichapwa mabao 7-0 na kabla ya hapo katika mzunguko wa pili msimu uliopita Simba ilishinda 5-1 na msimu huu wameichapa Yanga kwa mabao 3-1. Kocha wa Yanga Princess, Edna Lema alisema: “Yanga Princess ya sasa si ile ya zamani, mchezo hauamuliwi kwa historia, sina majeruhi kwenye kikosi, tumejiandaa vyema, mechi ni kubwa, tutapambana tushinde.”

Kwa upande wake, Mussa Mgosi ambaye ni kocha mkuu wa Simba Queens alitamba kuwa uchovu waliopata kwenye mechi iliyopita dhidi ya JKT Queens umeisha, hivyo watani zao wajiandae kupigwa tena kama kawaida.

“Tunahitaji pointi tatu tu si vinginevyo, tumejiandaa vizuri, tumefungwa mechi iliyopita tutamalizia hasira kwa watani. Wachezaji morali ipo juu, mashabiki waje kutuunga mkono,” alisema Mgosi.