Simba mjipange kwa Mtibwa

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba mpo? Mnaambiwa huko Manungu, benchi la ufundi la Mtibwa Sugar lipo kwenye mkakati maalumu wa kuhakikisha wanakichachisha kiporo cha Simba watakapowafuata kwao kuvaana katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Kocha Mkuu wa Mtibwa, Zubeiry Katwila amechimba mkwara kwa Simba kwamba hawatachomoka siku wakikutana nao katika mechi yao, kwa namna walivyojiandaa.

Alisema kama kuna mtu anadhani Yanga walifungwa kwa kubahatisha, basi wasubiri kuona kwa Simba.

“Sina maana Simba ni wabaya, ina wachezaji wazoefu wa hali ya juu, ila sisi ni kituo cha soka, muda wote tupo pamoja kambini, pia tunao wazoefu ambao wataisimamisha Simba,” alisema.

Katwila alisema wao hawawanii ubingwa kwa sasa, lakini hawatakubali kuona wanamaliza msimu wakiwa nafasi ya chini ndiyo maana wanaamua kukomaa na mechi zao ili wawe ndani ya Tano Bora.

Kocha huyo alifafanua kuwa, hawajipangi kuvuna alama kwa Simba watakaovaana mwezi ujao tu, ila ni kwa mechi zote ingawa anaafiki kwamba kwa hatua iliyofikia ligi kwa sasa kila mechi ni ngumu kwelikweli.

Mtibwa waliilaza Yanga 1-0 wiki iliyopita mjini Moro.