Simba kuogelea mamilioni SportPesa ikitwaa ubingwa Afrika

Muktasari:

Mbali ya fedha hizo, SportPesa pia imesema itaizawadia Simba kiasi cha Sh 100 milioni kama itafuzu hatua ya nusu fainali na Sh250 milioni endapo itatwaa ubingwa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Dar es Salaam. Kampuni ya michezo ya kubahatisha nchini, SportPesa imetangaza kuizawadia klabu ya Simba kitita cha Sh50 milioni baada ya kufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbali ya fedha hizo, SportPesa pia imesema itaizawadia Simba kiasi cha Sh 100 milioni kama itafuzu hatua ya nusu fainali na Sh250 milioni endapo itatwaa ubingwa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza jijini jana, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas alisema kuwa wamefarijika sana kuona Simba inafanya vizuri katika mashindano hayo.
Tarimba alisema kuwa wanaamini kuwa mafanikio ya Simba yametokana na chachu ya udhamini wao ambao pia wanaidhamini klabu ya Yanga.
“Hatua ambayo Simba imefikia ni kubwa na ya kujivunia. Kumbukeni kuwa Simba ni timu ya kwanza kuingia udhamini na SportPesa na baadaye Yanga kufuatia na Singida United. Lakini mpaka sasa, Simba imefanya mambo mengi ambayo sisi kama wadhamini wake tunajivunia sana,” alisema Tarimba.
Alisema kuwa wanaamini kuwa Simba itafanya vyema katika mashindano hayo na mengine yanayofuatia.
“Walipotwaa ubingwa wa Tanzania Bara wakiwa chini ya udhamini wetu, tuliwazawadia Sh milioni 100 na walipotinga fainali ya mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), tuliwazadia Sh milioni 50. Tunawapa hamasa wachezaji na benchi la ufundi la Simba...” alisema.