Simba kukiamsha bila Kagere, Chama

SERIKALI imetangaza kwamba michezo irejee kuanzia Juni mosi. Simba wamesisitiza kwamba wataingia vitani na kuchukua taji lao bila ya mastaa wao wanne ambao wako nje ya mipaka ya Tanzania.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mbata alisema kwa kauli ya serikali kurudisha ligi hawataweza kusubiri kuanza kazi wakiwasubiri wachezaji wao ambao wako nje ya nchi.

Wachezaji ambao wako nje mpaka sasa wa Simba ni kinara wa mabao katika ligi Meddie Kagere (Rwanda), viungo Clatous Chama (Zambia), Sharaf Shiboub (Sudan) na Francis Kahata (Kenya).

Senzo ameliambia Mwanaspoti kuwa kama mataifa hayo hayatakuwa yamefungua mipaka yao hawataweza kuwasubiri wachezaji hao ingawa wanatambua umuhimu wao katika kikosi chao.

Raia huyo wa Afrika Kusini alisema; “Ninawasiliana sana na hawa wachezaji wetu hata jana (juzi) nimeongea na wote kwa nyakati tofauti kujua maendeleo yao.

“Tunajua umuhimu wao lakini kama ligi ikianza sasa na uwezekano wa kuwapata ukiwa mgumu hatutaweza kuwasubiri, mambo lazima yaendelee hakuna namna.

“Tulisajili timu bora yenye jumla ya wachezaji 28 tutamalizia ligi kwa idadi ya waliobaki hakutakuwa na namna na malengo yetu yatakuwa yaleyale kuchukua ubingwa.

“Kwasasa tunasubiri taarifa ya jinsi gani ligi itaendeshwa wakati huu sisi wenyewe tukiendelea kujipanga kwa ndani kwa majukumu yetu,” alisema Senzo.

Wachezaji 23 wa Simba wako Jijini Dar es Salaam na tayari hivi karibuni kocha aliwaita na kuwapima afya na kuangalia hali zao tayari kuliamsha dude.