Simba, ulimwengu kaanza kutupia mabao js saoura

STRAIKA wa zamani wa TP Mazembe, Thomas Ulimwengu anayeichezea JS Saoura amefungua akaunti yake ya mabao Algeria kwa kuanza kutupia katika mchezo wa ligi dhidi ya Tadjenanet.

Tangu Desemba 25 mwaka jana ambapo Ulimwengu, alijiunga na JS Saoura alikuwa akiandamwa na ukame wa mabao katika michezo saba mfululizo ya mashindano yote.

Katika mchezo huo wa Jumamosi ambao Ulimwengu alitupia bao moja, JS Saoura iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ambayo yaliifanya kujikusanyia alama zote tatu.

Mechi hiyo ni ya nne kwa Ulimwengu ambaye alizaliwa Juni 14, 1993 kucheza kwenye ligi, mara yake ya kwanza ilikuwa Januari 4 ambapo timu yake ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Kabylie.

Akaja tena kupata nafasi kwenye michezo mingine dhidi ya MC Oran mchezo ulioisha kwa sare ya bao 1-1Januari 22 na Hussein Dey Februari 7 ambapo timu yake ilishinda bao 1-0.

Michezo mingine mitatu ambayo Ulimwengu aliondoka patupu ni ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba ya Tanzania, Al Ahly ya Misri na Vita Club ya DR Congo.

Ulimwengu mwenye umri wa miaka 25, ameshinda mataji mawili makubwa Afrika kwenye uchezaji wake soka akiwa na TP Mazembe ambayo ni Ligi ya Mabingwa, 2015 na Kombe la Shirikisho Afrika, 2016.

Kabla ya kujiunga na JS Saoura, Ulimwengu alikuwa akiitumikia Al Hilal ya Sudan. Simba bado ina mechi moja ya ugenini dhidi ya JS Saoura katika Ligi ya Mabingwa Afrika.