Shime atapamba kuwamaliza watoto wa Muswati

Muktasari:

Timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 ‘Tanzanite’ ipo  Afrika Kusini kama nchi mwalikwa kwaajili ya kushiriki mashindano ya COSAFA.

KOCHA  wa timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20 ‘Tanzanite’, Bakari Shime ametamba kuendeleza ushindi kwenye mchezo wao wa kesho Jumapili dhidi ya Eswatini  ili kutinga nusu fainali ya mashindano ya COSAFA, yanayofanyika Afrika Kusini.
Tanzanite ilianza kwa kishindo mashindano hayo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika, jana Ijumaa kwa kuifunga Botswana mabao 2-0, yaliyofungwa na  Opa Clement  huku lingine wakijifunga.
Shime amesema ushindi walioupata kwenye mchezo huo wa kwanza umewaongezea kujiamini zaidi wachezaji wake na kufanya vizuri  ambapo wataipigania nafasi ya kutinga nusu fainali dhidi ya Eswatini kabla ya kumalizana na Zambia, Agosti 6.
“Tutaingia na mbinu za kushambulia kama ilivyokuwa mchezo uliopita kwa lengo la kutafuta ushindi ambao utatuweka katika mazingira mazuri ya kuingia nusu fainali.
“Ushindi utatufanya tucheze bila kuwa na presha mchezo wetu wa mwisho tutacheza na Zambia, timu ilicheza vizuri dhidi ya Botswana na makosa yaliyojitokeza tumeyafanyia kazi,” amesema Shime.
Katika mchezo uliopita, Diana Msemwa wa timu ya Tanzanite alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na uwezo mkubwa aliyouonyesha Uwanja wa Gelvalande.
Michezo ya nusu fainali ya COSAFA chini ya umri huo inatarajiwa kuchezwa Agosti 8 ambapo kinara wa kundi B ambalo ipo Tanzanite atakutana na  timu iliyoshika nafasi ya pili kundi A huku timu iliyomaliza nafasi ya pili kundi B itacheza nusu fainali ya pili dhidi ya kinara wa kundi A.
Washindi michezo hiyo, watakutana fainali ambayo itachezwa uwanja wa Wolfson, Agosti 11 huku ikitanguliwa mechi ya mshindi wa tatu uwanja huo, Agosti 10.