Shiboub mtihani kwelikweli Simba

HUENDA kikosi cha Simba SC kikaendelea na michezo ya Ligi Kuu mwezi ujao bila ya kiungo wao, Shaaraf Shiboub kutokana na kile  kinachoendelea nchini kwao Sudan  katika kipindi hiki cha janga la virusi vya corona.

Awali kocha wa Simba SC, Sven Vandenbroeck alionekana  kuwa na hofu juu ya kurejea kwa kiungo wake huyo  Msudani, kwani hivi karibuni ilitangazwa marufuku ya wananchi kuzurula mitaani, ikiwa ni njia ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo.

Vandenbroeck alisema anaweza kuungana na Clatous  Chama ambaye yupo Zambia na Francis Kahata kutoka Kenya, lakini sio Shiboub ambaye nchini kwao kunaonekana kuwa na mkazo  wa hali ya juu wa marufuku ya kutoka ndani.

Kwa mujibu wa   Profesa Sadiq Tawor, mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Sudan,  anayeongoza kikosi kazi cha kupambana na ugonjwa huo aliyezungumza na Sauti ya Amerika (VOA), serikali nchini humo haikuwa na chaguo jingine isipokuwa kuweka kizuizi jumla.

“Hatua hii inachukuliwa kama moja ya jukumu letu kamili kwa usalama wa raia, kuwalinda kutokana na uzembe ambao unaweza kutokea,” alisema Tawor.

Wiki iliyopita serikali ilipiga marufuku safari zote kutoka Khartoum kwenda sehemu nyingine, lakini madereva wanaendelea na shughuli zao mbalimbali za kusafirisha watu kutoka mjini humo kwenda majimbo mengine. Tawor alisema tabia hiyo imechangia kuongezeka kwa kasi kwa corona.

“Kesi nyingi za maambukizi zilikuja kwa kuingiza watu binafsi kupitia nchi zingine, wale wanaosafiri kutoka Khartoum kwenda majimbo mengine. Wengine walipata kupitia usafirishaji wa kijamii, ambayo ni ukiukwaji wazi wa maagizo ya kiafya.”