Serengeti yaipa mzuka Stars

Muktasari:

Mbali na kusainiwa kwa mkataba huo, jezi mpya ambazo zitatumiwa na Taifa Stars kwenye mashindano mbalimbali msimu huu, zimezinduliwa rasmi na mashabiki wanaweza kuzinunua.

 

KAMPUNI ya Serengeti Breweries (SBL) imetoa udhamini wa miaka mitatu wa sh3 bilioni kwa Taifa Stars inayojiandaa na mashindano mbalimbali.

Taifa Stars itacheza Jumapili dhidi ya Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, lakini pia inakabiliwa na mashindano ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia, Mataifa ya Afrika na michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (Chan).

Serengeti imetoa udhamini mpya ukiwa ni ongezeko la sh900 milioni kutoka ule wa sh 2.1 Bilioni walioutoa miaka mitatu iliyopita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti, Mark Ocitti alisema; “Tumesaini tena mkataba huu baada ya kuridhishwa na mafanikio ya Taifa Stars kwa miaka mitatu iliyopita ikiwa ni pamoja na kufuzu AFCON mwaka jana ikiwa ni baada ya kupita miaka 39 tangu kushiriki mara ya mwisho.”

Naye Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) alisema; “Fedha hizi zitasaidia uendeshaji wa uhakika kwa Taifa Stars.”

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas alisema; “Fedha hizi zitumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa ikiwemo kuwapa huduma muhimu wachezaji ambao ndio walengwa wakuu.”