Sanchez, Lingard, Jones + Pereira = Sancho

Manchester, England. MANCHESTER United wanaendelea kuteseka baada ya Liverpool kubeba ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu England.

Ni miaka mingi kwelikweli, lakini mashabiki na mabosi wa Man United kamwe hawakupenda hilo litokee tena kwa mahasimu wao wakubwa, Liverpool.

Kutokana na hilo, bado wanakuna kichwa kukisuka upya kikosi cha Kocha Ole Gunnar Solskjaer ili msimu ujao kuingia kwenye ushindani wa kuwania taji hilo na sio kushiriki na kuwasindikiza wababe wenzao.

Ili kuongeza ushindani na kuingia kwenye mbio za ubingwa, Manchester United bado wanakomalia saini ya winga matata wa Borussia Dortmund, Jadon Sancho.

Tayari, Dortmund wameweka bayana kwamba, wanaweza kumuweka sokoni fundi huyo wa Kiingereza kama kuna timu itaweka mezani Pauni 110 milioni.

Kwenye orodha ya mastaa wapya wanaotakiwa na Solskjaer jina la Sancho lipo juu kabisa na ili kufanikisha mpango huo, Mashetani Wekundu wamekuja na mkakati mpya wa kuwapiga bei Alexis Sanchez na nyota wengine watatu ili kupata Pauni 110 milioni kumnasa Sancho.

Inaaminika kwamba kwa zaidi ya misimu miwili sasa, Manchester United wamekuwa wakifuatilia maendeleo ya Sancho na sasa wanamuona kama mtu sahihi wa kuongeza nguvu kwenye kikosi chao.

Habari za kuanimika zinaeleza kwamba, Solskjaer amemwambia makamu mwenyekiti wake Ed Woodward, kuwa atafute mkwanja kwa ajili ya kukamilisha dili la Sancho kwenye dirisha lijalo la usajili.

Hata hivyo, mara kadhaa Ed aliwahi kukaririwa akieleza kwamba, janga la virusi vya corona limetibua uchumi wa klabu hiyo hivyo, hawatarajii kufanya uhamisho wa pesa nyingi.

Mastaa ambao wanaweza kuwekwa sokoni ili kuvuna pesa na kupunguza bili za mishahara mbali na Sanchez anayelipwa Pauni 400,000 kwa wiki, wengine ni kiungo ambaye hasomeki Jesse Lingard, Andreas Pereira na mabeki wa wiwili wa kati Phil Jones na Chris Smalling aliyepo kwa mkopo AS Roma ya Italia.