Samatta atumia saa 38 dakika 8 kumwomba radhi baba yake

Muktasari:

  • Mbwana Samatta anatumia gharama kubwa ya kumuangukia baba yake mzazi anayejulikana kwa jina la Ally Samatta Pazi, inapotokea amekiuka masharti aliyompangia kuyafanya katika kazi yake ya mpira wa miguu.

ANACHOKIFANYA baba mzazi wa Mbwana Samatta kinaonekana kama kichekesho vile, lakini ndani yake kina maumivu makali kinampotezea muda mwingi supastaa huyo anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji.

Ipo hivi. Mzazi wa staa huyo, Ally Samatta Pazi, aliwaonya watoto wake Mbwana anayekipiga (Genk) na Mohammed (Mbeya City) wasipende kuwa kimbelembele kupiga penalti kwa madai hawana ufundi huo na mara kadha anawaona hawazimudu na wakati mwingine kuzigharimu timu zao, jambo alilosema linamkasirisha sana.

Juzi Jumapili sasa, Taifa Stars ilicheza na Cape Verde Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mechi ya marudiano ya kufuzu fainali za AFCON, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, yaliyofungwa na Simon Msuva anayecheza Difaa El Jadida ya Morocco na Mbwana ambaye kabla ya kutikisa bao la pili alikosa penalti, hapo ndipo kisanga na baba yake mzazi kilianza.

Licha ya Samatta kufunga bao la pili, baba yake mzazi hakupendezewa na mwanaye kukosa penalti na kwamba huenda Stars ingeibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Mzee huyo alifichua inapotokea Samatta na Mohamed wakakosa penalti hataki pesa ambazo aliwapangia wamlipe watume kwenye simu, badala yake wanatakiwa kusafiri na kumfuata alipo.

Saa 38 dakika 8 ya adhabu

Adhabu hiyo inaonekana kumuumiza zaidi Mbwana anayecheza Ubelgiji kwani anatumia muda wa saa 38 na dakika 8 kutoka Ubelgiji mpaka jijini Dar es Salaam anakoishi baba yake ili kumpatia pesa ya kukosa penalti ambapo awali alikuwa anatoa Sh 5,000 lakini sasa adhabu hiyo imepanda hadi kufikia Sh 10,000. “Awali niliwaambia watakuwa wananilipa Sh 5000, lakini bado wanaendelea kupiga penalti ovyo, nimeongeza kiasi itakuwa Sh10,000 natafuta na adhabu kali zaidi itakayowafanya wawe makini ama wawaachie wengine zoezi hilo, napenda vijana wangu wawe mfano dhidi ya wengine kwani hata mimi zamani nilikuwa mfano dhidi ya wachezaji wenzangu,” alisema Mzee Samatta.

“Unajua hata mashabiki wanajua ni nani hawezi kukosa penalti yupo mtu kama Erasto Nyoni, anapoenda kupiga unamuona jinsi anavyomsoma kipa na anaonyesha ujasiri wa kupatia, katika eneo hilo natamani wawe hivyo lakini sio kukosa kosa,” alisema.

Euro 2,084

Samatta anatumia ndege ya KLM kwenda Ubelgiji na kurudi Dar es Salaam, ambapo kwa daraja analopanda anatumia Sh 5,522, 000 (kwenda na kurudi) sasa inapotokea amepatikana na adhabu ya kukosa penalti hicho ndicho kiasi anacholazimika kutumia nje na matumizi yake ya njiani na anapofika nyumbani kwao.

Mzee huyo alifichua siri nzito kwamba alipokuwa anataja kiasi hicho, Mbwana na Mohammed waliona ni jambo la kawaida na hawakuwaza usumbufu wanaoweza kuupata.