Samatta, Chilunda kutua leo, Stars yaingia mafichoni

Muktasari:

  • Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi alisema wachezaji wengine wanaocheza ligi za nje ya nchi wamejiunga na timu hiyo tokea siku ya kwanza ya kambi.

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta anayechezea KRC Genk pamoja na Farid Mussa na Shaaban Chilunda wanataraji kuwasili wakati wowote kuanzia na wenzao tayari kwa ajili ya mechi ya mwisho ya kufuzu mashindano ya mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Uganda, The Cranes.

Ujio wa Samatta, Chilunda na Mussa unakamilisha idadi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakiwa tayari wameanza mazoezi na Taifa Stars kujiandaa na mechi dhidi ya Uganda Machi 24 kuanzia saa 1.00 usiku.

Wakati Chilunda anachezea timu ya Deportivo Izarra kwa mkopo, Mussa anakipiga katika timu ya Deportivo Tenerife B ina zote zikicheza katika ligi ya Segunda daraja B.

Msangi alisema kuwa wachezaji Shiza Kichuya anayeichezea ENPPI SC ya Misri na Himid Mao  wa Petrojet SC walitarajia kujiunga na timu hiyo leo usiku na kesho watafanya mazoezi na timu kwenye uwanja wa Boko Beach Veteran.

Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi alisema wachezaji wengine wanaocheza ligi za nje ya nchi wamejiunga na timu hiyo tokea siku ya kwanza ya kambi.

Wachezaji hao na klabu zao kwenye mabano ni Yahya Zayd (Ismaily), Hassan Kessy (Nkana FC), Thomas Ulimwengu (JS Saoura, Algeria), Simon Msuva (Diffaa El Jadida) na Rashid Mandawa anayechezea BDF FC ya Botswana.

Alisema kuwa wachezaji wote wa nyumbani pamoja na wale wa Simba ambao leo wanacheza na timu ya Ruvu Shooting katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara wapo kambini. Wachezji hao ni Aishi Manula, Erasto Nyoni, Jonas Mkude na John Bocco.

“Morali ya kambi ipo juu kila mchezaji anataka kupigania taifa lake katika mechi hiyo. Ndiyo maana wachezaji wengi wamewasili tarehe rasmi ya kambi iliyopangwa,” alisema Msangi.

Alisema lengo ni kufuzu fainali za Afcon zilizopangwa kufanyika Misri kuanzaia Juni 21 mpaka Julai 19. Taifa Stars ipo nafasi ya tatu kwa ikiwa na pointi tano pamoja na Lesotho ambayo ipo nafasi ya pili kwa idadi ya pointi hizo hizo.

Lesotho itacheza na Cape Verde yenye pointi nne. Timu tatu zote zinaweza kuungana na Uganda ambayo tayari imefuzu hatua ya fainali.