Safari ya Lema Bundesliga imeiva

Monday February 18 2019

 

NDOTO ya winga wa Kitanzania, Michael Lema kucheza soka Ujerumani huenda ikatimia majira ya kiangazi baada ya kuwepo taarifa kuwa mtafuta vipaji wa Beyern Munich, Wolfgang Grobe yuko mbioni kuelekea Austria.

Lema mwenye ndoto ya kucheza Ligi Kuu Ujeruman ‘Bundesliga’, alisema amepokea taarifa kutoka kwa wakala wake kuhusu ujio wa Grobe pande za Austria.

Grobe ni mchezaji wa zamani wa Kijerumani ambaye enzi zake alitesa akiwa na Eintracht Braunschweig na FC Bayern Munich kabla ya kutundika daruga na kusomea ukocha kisha kugeukia kazi ya utafutaji vipaji Juni 2011.

“Kocha wangu wa timu za vijana za SK Sturm Graz aliwahi kufanya kazi Bayern Munich, niliwahi kumuuliza uwezekano wa kujiunga na timu yao ya vijana, alinieleza utaratibu ni tofauti na timu nyingine za Ujerumani.

“Nilipuuzia inshu za kujipeleka Bayern na badala yake nikaongeza nguvu kwenye kujituma ili nipandishwe kikosi cha kwanza ili uwe kama mwanya wa kuonekana zaidi,” alisema Lema.

Winga huyo kumbe wakati akiwa na timu za vijana ambazo zimezoeleka kwa wenzetu kushiriki ligi mbalimbali za madaraja ya chini alikuwa akifuatiliwa na Grobe.

Lema amekuwa na msimu mzuri akiwa na kikosi cha vijana amecheza michezo 12 na amefunga mabao 13 kwenye Ligi Daraja la Tatu Austiria.

Akiwa na kikosi cha kwanza cha SK Sturm Graz kwenye michezo mitano ya Ligi Kuu amefunga bao moja.

Advertisement