Sababu za David Ospina kuzimia uwanjani ni hizi

Muktasari:

Majeraha haya ni madogo lakini yanaweza kuwa na matokeo mabaya kwa aliyejuruhiwa ikiwamo maumivu makali ya kichwa, kutojitambua kuweweseka au kupoteza fahamu.

David Ospina Golikipa wa Arsenal ya Uingereza ambaye yuko kwa mkopo Napoli ya Italia siku ya Jumamosi alipatwa na ajali mbaya ya kichwani, baada ya kugongana na mchezaji wa Udinese.

Ilikuwa ni katika kipindi cha kwanza golikipa huyu wa kimataifa wa Colombia aligongana na kiungo wa Udinese, Ignacio Pusseto na kujeruhiwa eneo la kichwani

Alitibiwa na kufungwa bandeji kichwani na ingawa aliendelea na mchezo huo mpaka alipoteza fahamu ghafla baada ya kupita nusu saa.

Hali hii ilisababisha kupewa huduma maalumu ya dharura uwanjani na baadaye alitolewa nje na kuwahishwa katika huduma za afya kwa matibabu na uchunguzi zaidi.

Imeelezwa kugongana huko kulimsababishia mtikisiko wa ubongo hali inayojulikana kitabibu kama Concussion. Aina hii ya jeraha la ubongo ndilo linahusishwa na kupoteza fahamu kwa kipa huyu.

Tayari ameishafanyiwa vipimo vya skani ya ubongo na imeonekana ni mtikisiko tu wa ubongo hakuna mchaniko wa ubongo au kuvilia damu katika ubongo.

Tatizo hili alilolipata limewahi kumpata kipa wa sasa Arsenal Petr Ceck na kipa wa zaman wa Liverpool Karius.

Leo tutaona majeraha ya kichwani ambayo makipa hawa wamekuwa wahanga kutokana na kugongana na washambuliaji wakijaribu kuokoa hatari za langoni.

Taarifa za jumla ya majeraha ya kichwa

Majeraha ya kichwa ni majeraha yanayotokana na kajeruhi nyama za nje ya kichwa, mfupa wa fuvu na ubongo. Majeraha haya yanaweza kuwa madogo, ya kati na makubwa.

Hatari ya kuweza kupoteza maisha ni pale inapotokea umejeruhiwa katika ubongo na kuvujisha damu ndani kwa ndani au likawa ni jeraha lililochana au kupasua mfupa wa fuvu la kichwa na kujeruhi ubongo.

Majeraha ya kichwani yanaweza yakaletwa kwa kupigwa na kitu butu kama ilivyomtokea Ospina baada ya kugongwa kichwani.

Kuna aina karibu tatu za majeraha ya kichwa kijumla, aina ya kwanza ni concussion ambayo ndiyo aliyoipata Ospina. Ni hali ya ubongo kupata mtikisiko na kusababisha kuvurugika kwa ufanisi wa ubongo na kupoteza fahamu dakika chache tangu kugongwa kichwani.

Majeraha haya ni madogo lakini yanaweza kuwa na matokeo mabaya kwa aliyejuruhiwa ikiwamo maumivu makali ya kichwa, kutojitambua kuweweseka au kupoteza fahamu.

Aina ya pili ni contusion maana yake nikuwa tishu za ubongo zimepata vi michubuko au vijeraha vidogo kiasi cha kuweza kuvujisha damu kwa mishipa midogo iliyojeruhiwa.

Jeraha la aina hii hutokea pale ubongo unapopata shinikizo kubwa kwa kugongana na kitu kizito.

Aina ya tatu ambayo ni mbaya zaidi ni brain laceration hii inatokea tishu ya ubongo imechanika au kukwanyuka.

Mara nyingi ajali kama aliyopata kipa huyu hatari ya huambatana na damu kuvuja na kuvilia ndani huwa ni kubwa, na inapotokea huvuruga ufanisi wote wa ubongo.

Maumbile ya kichwa yalivyo na kazi zake

Kichwa huwa na sehemu tatu yaani nyama laini ikiwamo ngozi iliyofunika misuli na nyama laini, mfupa wa fuvu na ubongo.

Nyama laini hufunika mfupa wa fuvu, ambao nao hufunika ubongo na kuulinda usidhuriwe na kitu chochote.

Ubongo ndio mdhibiti wa shughuli mbalimbali, ndio maana inapotokea sehemu fulani katika ubongo imepata jeraha na kuharibika kunaweza kukusababishia matatizo makubwa.

Ubongo ukijeruhiwa madhara yanayoweza kujitokeza ni kama vile kupooza mwili au eneo lolote la mwilini, kushindwa kuzungumza au kupoteza kumbukumbu zote.

Kupoteza fahamu ni moja ya mbinu ya mwili kujihami dhidi ya majeraha ya ubongo.

Mwili unapopoteza fahamu huzima shughuli zingine na kujikita katika maeneo nyeti ikiwamo ubongo wenyewe ili kusahihisha na kujaribu kufanya utatuzi baada ya kujeruhiwa na kupoteza ufanisi.

Na hii ndio maana baada mjeruhiwa anaweza kurudiwa na fahamu kama ilivyotokea kwa Ospina fahamu zilirudi hapo baadaye na mwili ukaendelea na kazi zake kwa kawaida.

Kupoteza fahamu kwa muda mfupi ni moja ya ishara kuwa jeraha alilopata si kubwa sana bali ni mtikisiko tu wa ubongo.

Kituo kikuu cha udhibiti wa mfumo wa upumuaji kipo katika Ubongo sehemu ya nyuma, inapotokea mtikisiko wowote wenye shinikizo kubwa unavuruga ufanisi wa ubongo.

Namna majeraha ya kichwani yanavyotibiwa

Majeraha ya kichwa ni hatari ambayo kama hatua za haraka hazitachukuliwa majeruhi anaweza kupoteza maisha ndiyo maana mmoja wa Daktari aliyekuwa anampa huduma Ospina uwanjani alitoa ishara ya kuhitaji wasaidizi zaidi kumhudumia.

Majeruhi huweza kupatiwa huduma ya kwanza pale pale mahali alipodondokea ikiwamo kuweka katika ulalo sahihi, kuimarisha njia ya hewa na kupewa hewa ya oksijeni, upumuaji saidizi na mzunguko wa damu. Uchunguzi wa pale pale hufanyika wa kimwili ili kutathimini viashiria vya majeraha makubwa ya kichwani vilivyojiitokeza.

Alipewa huduma ya kwanza pale pale alipopata ajali na kubebwa kwa vifaa vyevye usalama wa kutosha na kutolewa nje ya uwanjani kwa huduma zaidi.

Kuwahi kupelekwa katika hospital kubwa kwa ajili ya matibabu ni mojawapo ya jambo linaweza kuokoa maisha ya majeruhi ya kichwa kwani huduma atakazopata zinaweza okoa maisha.

Uchunguzi wa kwanza muhimu wa haraka ni kupata picha ya CT Scan ili kubaini haraka kama kuna tishu za ubongo zimejeruhiwa au kuna damu inayovuja.

Ct scan ni mashine maalum ya uchunguzi wa tishu za mwilini inayotumia picha za Computer na kuonyesha taswira ya tishu laini.

Ikibainika kuwa damu imevuja hatua za kuiondoa haraka damu hiyo kwa njia za upasuaji hufanyika kwani inapovilia ni hatari kwa tishu za ubongo na kifo kinaweza kutokea.

Namna ya kupunguza hatari ya majeraha ya kichwa

Ni vigumu kuzuia kutokea kwa ajali kama hizi kutokea katika mchezo wa soka. Habari nzuri ni kuwa makipa huwa wanalindwa na sheria za soka wanapokuwa katika eneo la 18 na ndiyo maana hata wakati kinyang’anyiro ukimgusa kipa huwekwa faulo.

Majeraha ya aina hii yanaweza kupunguzwa kwa kuwavisha kifaa tiba yaani kofia maalum kuwakinga wasijijeruhi tena kama kifaa anachovaa Petr Check golikipa wa Arsenal.

Mtikisiko wa ubongo ndiyo ulimfanya Ospina kuzimia ila kwa sasa anaendelea vizuri na amepewa mapumziko huku akiwa katika uangalizi wa karibu wa wataalam wa Afya.