Saa 72 za msimamo Ligi Kuu ni balaa zito

WAKATI kikao cha serikali juu ya mikakati ya Ligi Kuu kikiingia siku ya tatu leo, bado kumekuwepo sintofahamu juu ya kituo ambacho mechi hizo zitachezwa licha ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe wiki iliyopita kueleza kuwa Ligi Kuu itachezwa Dar es Salaam.

Juzi Jumamosi, jana Jumapili na Leo Jumatatu, serikali kupitia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo imekuwa na kikao kizito kujadili namna Ligi hiyo itakavyorejea, baada ya matukio ya kimichezo kuruhusiwa kutimua vumbi tena Juni Mosi baada ya kusimama tangu Machi 17 kwa lengo la kusitisha mikusanyiko ili kuchukua tahadhari ya janga la corona.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo ameliambia Mwanaspoti kuwa bado majadiliano yanaendelea na wanatarajia leo Jumatatu ndipo kuhitimisha kikao chao juu ya mustakabali wa namna michezo itakavyorejea ikiwamo Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, la Pili na Kombe FA ambazo ndizo Dk Mwakyembe amezitaja kuwa zitaanza baada ya Rais John Magufuli kuruhusu matukio ya kimichezo nchini.

“Jana hatukumaliza majadiliano, tuliwaita watu wa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na Bodi ya Ligi ambao walikaa kwenye kikao kidogo na kuondoka tukabaki kwenye majadiliano ya kiserikali,” alisema juzi Jumamosi walijadili muongozo wa michezo yote kabla ya kujadili ule wa Ligi.

“Leo (jana) tutafanya maboresho na kesho (leo) tutakamilisha muongozo mkubwa,” alisema Singo ingawa habari za ndani zinasema Bodi ya Ligi wameshikilia msimamo wa kutokuwepo kwa mashabiki kabisa viwanjani hata wale 10 waliotajwa.

Licha ya kuwepo taarifa kuwa Bodi ya Ligi haikushirikishwa katika mchakato wa kupanga Ligi Kuu ichezwe jijini Dar es Salaam, Singo amesema maelekezo yaliyopo mpaka sasa ni Ligi Kuu na FA kuchezwa Dar es Salaam kama alivyoelekeza Waziri.

“Mpaka sasa hakuna mabadiliko yoyote katika hilo,” alisema Singo na kuongeza, kama kutakuwa na mabadiliko itaelezwa baada ya kikao cha kesho (leo), ingawa taarifa za awali za Waziri za wiki iliyopita hazijabadilika.

“Tulijadili pia kuhusu michezo mingine ni vipi itaruhusiwa kuendelea, kikao kilimalizika usiku na leo (jana) tunaendelea tena na kesho (leo) tunatarajia kuhitimisha na kutoa taarifa rasmi,” alisema.

Licha ya kauli hiyo ya Singo, Mwanaspoti limedokezwa kuwa mpango wa Ligi Kuu kuchezwa jijini Dar es Salaam ni jambo ambalo liliteka mkutano huo kati ya serikali na bodi ya ligi kwenye kikao cha juzi Jumamosi.

“Bodi nayo ilitaka Ligi ichezwe kwenye kituo kimoja, lakini ni wapi ilikuwa bado haijaamuliwa na walitaka kuzishirikisha na klabu, ingawa tayari waziri amesema ni Dar es Salaam, mvutano ndipo uko hapo,” alisema mtoa taarifa wetu kutoka kwenye kikao hicho ambaye aliomba asitajwe.

Alisema kila kitu kinakwenda sawa, isipokuwa ni mkoa gani Ligi ichezwe, hapo ndipo kwenye mgongano,” alisema mtoa taarifa wetu huyo.

Hata hivyo, Ligi inaanza kati ya Juni 10 au 15 ambapo zitachezwa mechi zote za viporo hadi kila timu ifikie mzunguko 29 kabla ya zote kuendelea kwa tahadhari kubwa ikiwamo wachezaji kupimwa, timu kucheza bila mashabiki pamoja na wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi kukaa mbalimbali.