SIO ZENGWE: Sakata la Morrison mtihani wa uadilifu kwa TFF

Muktasari:

Kama Yanga wana mkataba ambao ni halali, yule aliyepeleka TFF mkataba wa kughushi, atalazimika kushughulikiwa kwa mujibu wa kanuni

KAMA kuna jambo ambalo viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanatakiwa kuonyesha uadilifu wa hali ya juu, ni katika sakata la mchezaji machachari kutoka Ghana, Bernard Morrison.

Hili ni suala ambalo mwamuzi pekee anayewesha kuheshimiwa ni mahakama ya kawaida baada ya kutumbukia katika suala linaloweza kuonekana kuwa dogo, lakini ni kubwa sana iwapo upande mmoja utakomaa.

Hili ni suala la mkataba feki. Morrison anadai na ameshapeleka TFF madai kuwa mkataba uliopo sasa ni sahihi kwa kuwa hajasaini mkataba wowote wa kuongeza muda katika klabu ya Yanga zaidi ya ule wa miezi sita anaoutambua.

Yanga inadai mchezaji huyo wa kiungo ana mkataba wa miaka miwili aliosaini kabla ya ule wa miezi sita kuisha, hivyo ni mchezaji halali wa klabu hiyo ya Jangwani.

Siliangalii sana suala kwamba Mghana huyo amesaini mkataba mwingine Simba, kwa kuwa hilo halina jinai zaidi ya taratibu za kawaida za kisheria ndani ya duru za soka.

Lakini mzozo huo kutumbukia katika kuwepo kwa mkataba feki, ni suala zito ambalo TFF kwa uwezo ilionao haiwezi kufikia muafaka wa juujuu na kufanya majumuisho kuwa kulikuwa na mkataba feki, hivyo Morrison alikuwa huru kusaini mkataba klabu nyingine.

Maana yangu ni kwamba iwapo kutabainika kulikuwa na mkataba wa kughushi, TFF haitatakiwa iishie eti katika kusema Morrison yuko huru, bali kuanza kulishughulikia suala hilo kimaadili.

Kwanza ni lazima vyombo vilivyo na dhamana ya kushughulikia jinai ya kughushi vihusishwe ili kubaini kama kulikuwa na kosa hilo. Ni dhahiri kuwa vikibaini ni lazima aliyehusika ashughulikiwe kisheria, kwa kuwa kisheria hilo ni kosa kubwa.

TFF ni lazima ijue na baadaye kuweka hadharani kuwa ni nani alighushi mkataba huo? Aliyeghushi ni lazima afikishwe mbele ya vyombo vya kimaadili vya TFF kujieleza na akibainika ana kosa, basi adhabu zilizoelezwa katika kanuni za maadili ni lazima zimkute muhusika.

Na kanuni za maadili haziishii hapo tu, zinaitaka TFF kulifikisha suala hilo katika mamlaka za nchi ili liadhibiwe kwa mujibu wa sheria.

Kama Yanga wana mkataba ambao ni halali, yule aliyepeleka TFF mkataba wa kughushi, atalazimika kushughulikiwa kwa mujibu wa kanuni za maadili za TFF na baadaye katika mamlaka za kisheria za nchi.

Kuna jambo jingine la ajabu. Inakuwaje mchezaji ambaye hakusaini mkataba, akawa na nakala ya mkataba wa kughushi? Aliipataje nakala ya kughushi, akijua hakusaini mkataba?

Ukiachana na vimbwanga hivyo, TFF ina kazi ya kufanya iwapo itathibitika kuwa mkataba huo haukuwa wa kughushi. Simba imeonyesha Morrison ameshasaini mkataba na klabu hiyo. Ni kina nani walihusika na mazungumzo ya kumshawishi asaini mkataba?

Na ilikuwaje Simba wakaingia mkataba na mchezaji ambaye mzozo wake bado unashughulikiwa na TFF? Hapo kuna suala la kuvujisha siri za vikao vya TFF vinavyoshughulikia suala hilo. Yaani ni lazima Simba walitonywa kuwa—kama ni kweli—kwamba Morrison hana mkataba mwingine Yanga, au tayari TFF imeshabaini Mghana huyo hafungwi Yanga.

Kama ilibainika hivyo, basi kuna wajumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, ambayo ilikuwa inashughulikia suala hilo, walivujisha siri kwa Simba ili waendelee na mikakati yao hata kabla ya kamati hiyo kutangaza uamuzi kuhusu suala hilo.

Hali kama hiyo iliwahi kujitokeza wakati wa Athuman Chuji na Kelvin Yondani, lakini mamlaka husika hazikuchukua hatua zinazostahili.

Binafsi naona kuna maswali mengi kuhusu sakata hilo, huku viongozi wa Simba wakiwa wamemtoa mhanga Haji Manara ndio aonekane peke yake anahusika na Morrison, wengine wakijificha.

Lakini sakata hilo ni mtihani mkubwa wa uadilifu kwa uongozi wa sasa wa TFF. Ni suala ambalo likichezewa, linaweza kusababisha watu kurejesha ule mtindo wa kukimbilia mahakamani kwa kuwa uongozi hautendi haki inavyostahili.

Ni muhimu TFF ikajipambanua uadilifu wake katika kushughulikia suala hili, la sivyo inaweza kushuhudia vile vituko vya zamani vikarejea na baadaye kukawa na aibu kubwa kwa nchi.