Runinga zihusike mechi za mchujo

KUNA mechi za mchujo zimeanza, zikihusisha baadhi ya timu kwa ajili ya kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao lakini pia zile zinazowania kubaki Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Kwa timu zinazowania Ligi Kuu, klabu nne za Ligi Daraja la Kwanza ambazo ni Mlale FC, Geita Gold, Mbeya Kwanza na Pamba zenyewe zitapambana kusaka nafasi mbili za kucheza dhidi ya timu za Ligi Kuu ambazo zitashika nafasi ya 17 na 18 kwenye msimamo mwishoni mwa msimu kwa ajili ya kupigania nafasi ya kucheza Ligi Kuu.

Kwa upande mwingine, timu nne za Ligi Daraja la Kwanza ambazo ni Transit Camp, AFC, Ashanti United na Dar City zenyewe zitapigania nafasi tatu za kubaki Ligi Daraja la Kwanza.

Kuanzia mechi za kuwania kubaki Ligi Daraja la Kwanza na zile za kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao, zote zina maana kubwa na zinapaswa kupewa umuhimu mkubwa katika kipindi hiki pengine kuliko kipindi kingine chochote.

Tukumbuke kuwa hiki ni kipindi ambacho klabu hizo kila moja inapigania uhai wake, iwe kwa zile zinazopambana ili ziende Ligi Kuu msimu ujao na zile ambazo zinapambana ili kujinusuru na janga la kushuka.

Ni wazi kwamba nguvu kubwa ya timu hizo itaelekezwa kwenye mechi za mchujo kwa sababu zinachezwa chache na timu yoyote ambayo itashindwa kuchanga vyema karata zake itajikuta ikishindwa kutimiza lengo lake.

Kuna uwezekano mkubwa mipango hiyo ya timu husika ikagubikwa na mbinu za hila na hujuma ilimradi tu timu hizo zipate matokeo mazuri ambayo yatazisaidia kufanya kile ambacho zinategemea kukipata.

Kutokana na hilo, ni vyema Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kama vile Jeshi la Polisi pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) vikafuatilia kwa umakini wa hali ya juu mechi hizo za mchujo ili wapatikane washindi halali.

Kumekuwapo na malalamiko ya kutosha kuhusiana na Ligi Daraja la Kwanza kuwa imeshamiri vitendo vya hujuma ambavyo vimekuwa vikifanywa na timu, hivyo hatua zisipochukuliwa hata hizi mechi za mchujo zinaweza kugubikwa na jinamizi hilo. Na mbali ya TFF, Bodi ya Ligi pamoja na Takukuru kuzitupia jicho mechi hizo, suluhisho jingine la haraka ni kuruhusu mechi hizo zionyeshwe kwenye runinga ili kutengeneza mazingira mechi hizo kuchezeshwa kwa haki na usawa.

Ili soka lipige hatua ni lazima tuwe na ligi au mashindano ambayo washindi wanapatikana kihalali na siyo kwa njia za ujanjaujanja, fitina pamoja na ubabaishaji ambazo zimekuwa hazijengi, bali hubomoa.

Lakini bado huwezi kujisifia kuwa una ligi bora kama hadi suala la mechi kuonyeshwa kwenye runinga linakuwa gumu iwe kuonyeshwa moja kwa moja au kurekodiwa. Tulitazame hili kwa jicho pevu, bado hatujachelewa.