Robin van Persie asimulia bao lake lililoipa Man United ubingwa

Muktasari:

Van Persie alisema bao hilo ndilo bora kabisa katika maisha yake kwenye kikosi cha Man United huku akifichua kwamba walianza kuchati na Wayne Rooney kabla ya kufunga bao hilo.

MANCHESTER, ENGLAND .ROBIN van Persieeeeeee! Ukisikia hivyo tu, ujue wanaokota kwenye nyavu huko.

Ilikuwa homa ya makipa hiyo kwenye Ligi Kuu England wakati alipokuwa akifanya biashara yake ya kutikisa nyavu akiwa na kikosi cha Arsenal na Manchester United.

Huyu ni straika wa Kidachi, Robin van Persie maarufu kama RVP.

Straika huyo aliduwaza wengi wakati alipohama kutoka Arsenal kwenda kujiunga na Man United kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwaka 2012. Haikuwa ngumu kwa kocha Arsene Wenger kumuuzia silaha mpinzani wake, Sir Alex Ferguson. Lakini, hakukuwa na namna, Van Persie hakuwa tayari kuongeza dili jipya la kubaki Arsenal na Man United walikuwa tayari kutoa Pauni 24 milioni kunasa huduma ya mshambuliaji huyo. Biashara ikafanyika.

Baada ya kutua Man United, msimu wake wa kwanza tu, Van Persie alifunga mabao 30 na kuipa miamba hiyo ya Old Trafford taji la Ligi Kuu England, lakini straika Van Persie alisema kwamba mabao yake yote aliyofunga, lile alilowachapa Aston Villa, lililowapa ubingwa lilikuwa bonge la bao.

Van Persie alisema bao hilo ndilo bora kabisa katika maisha yake kwenye kikosi cha Man United huku akifichua kwamba walianza kuchati na Wayne Rooney kabla ya kufunga bao hilo.

Hakuna ubishi, kiwango binafsi cha straika huyo kwenye msimu wa 2012-13, ndicho kilichoipa ubingwa wa ligi Man United, taji ambalo la mwisho kubeba kwenye ligi hiyo hasi sasa, ambapo kwa kipindi hicho walikuwa chini ya kocha Sir Alex Ferguson.

Van Persie alifunga kwa mpigo wa ‘volley’ kufuatia pasi ndefu ya mchinja kutoka kwa Rooney. Lakini, RVP anafichua kwamba bao hilo lilifungwa baada ya kuchati kwanza kabla ya mpira kuanza namna ya kuwaduwaza mabeki wa Aston Villa, hasa kwenye mchezo huo, ambapo Man United ilifahamu kwamba ushindi ungewafanya kubeba taji.

“Kulikuwa na nyakati nyingi sana tamu pale Man United, lakini nyakati tamu zaidi ni zile za usiku tuliobeba ubingwa baada ya mechi ya Aston Villa,” alisema.

“Nikitazama nyakati zote kwenye maisha yangu ya mpira, usiku ule unazidi nyakati zote.

“Man City walikuwa wamepoteza mechi dhidi ya Tottenham siku moja iliyopita, hivyo kama tungeshinda dhidi ya Asto Villa basi hakuna timu ambayo ingetufikia. Nilienda Man United kushinda ubingwa wa ligi. Hivyo huo ulikuwa wakati wetu wa kutimiza lenga.

“Kulikuwa na hisia kama tunacheza fainali zile. Asubuhi kabla ya mechi hiyo, uliweza kuona kwenye nyuso za wachezaji, kila mtu alionekana kuwa na furaha na kutambua kilichokuwa kinakwenda kutokea.

“Hata kama tungepoteza, bado tulikuwa na mechi nne mbele za kufanya hivyo, lakini tulitaka kumaliza msimu ndani ya usiku huo, tena mbele ya mashabiki wetu. Mambo yalikuwa yamejiweka vizuri.

“Nilifunga bao la kwanza baada ya dakika mbili tu, nilimalizia tu wavuni kupitia pasi ya Giggsy. Baada ya hapo, nilipata hisia kwamba, Ok, leo inakwenda kuwa siku nzuri.

“Nadhani unajua ninachokimanisha. Nilikuwa na hisia kali ya furaha. Bao la kwanza lilituondoa presha na baada ya hapo mchezo ulikuwa upande wetu.

“Sura za wapinzani wetu, zilikuwa zikionyesha kwamba hawakuwa na cha kupoteza, tena kwa usiku huo.

“Kabla ya mechi, Wayne na mimi tulizungumza, tulizungumza namna ya kuwawahi mabeki wa Aston Villa, nilimwambia apige pasi fasta akiniona nipo nyuma ya mabeki wa Aston Villa. Hiyo ndiyo njia tuliyotumia kuwaadhibu wapinzani.

“Unapokuwa na wachezaji kama Wayne, Carrick, Scholesy wanacheza nyuma yao, unafahamu muda wowote pasi inakufikia. Hicho kilikuwa kitu kizuri sana.”

Van Persie aliondoka Man United 2015 kwenda kujiunga na Fenerbahce ya Uturuki, alikocheza kwa miaka mitatu kabla ya kwenda kujiunga na Feyenoord ya kwao Uholanzi, alikocheza kwa mwaka mmoja kabla ya kutundika daruga. Feyenoord ndiyo timu yake ya utotoni iliyompa nafasi ya kucheza soka la kulipwa. Kwenye mchezo huo dhidi ya Aston Villa, Man United iliishinda mabao 3-0, mabao yote ya Robin van Persie.