Rasta anakuja dirisha dogo

Yacouba Songne,

Muktasari:

Kocha huyo amesema kama si kufungwa kwa dirisha la usajili wa Ligi Kuu Bara, basi mtu wa kwanza kumnyakua kikosini kwake angekuwa Yacouba Songne, yule rasta wa Asante Kotoko aliyeupiga mpira mwingi juzi Jumatano pale Uwanja wa Taifa.

HIVI unapoisoma habari hii fahamu kuwa kikosi cha Simba kipo njiani kuelekea Lindi kwa mchezo wa kirafiki wa kuzindua Uwanja wa Namungo uliojengwa kwa nguvu za Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, lakini huku nyuma Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, amefichua jambo.

Kocha huyo amesema kama si kufungwa kwa dirisha la usajili wa Ligi Kuu Bara, basi mtu wa kwanza kumnyakua kikosini kwake angekuwa Yacouba Songne, yule rasta wa Asante Kotoko aliyeupiga mpira mwingi juzi Jumatano pale Uwanja wa Taifa.

Straika huyo raia wa Burkina Faso, alionyesha kiwango cha hali juu katika pambano la kimataifa la kirafiki la Simba Day kati ya Simba na Kotoko na Aussems amesema kama atahitaji straika mpya, basi Yacouba atakuwa pendekezo la kwanza.

Kocha huyo aliyasema hayo mara baada ya pambano hilo lililomalizika kwa sare ya bao 1-1 kwa kusema kwa soka alililopiga Yacouba, kocha yeyote makini angetamani kuwa naye kikosini mwake.

Alisema Yacouba aliyewasumbua Pascal Wawa, Erasto Nyoni na James Kotei, huku akimtesa Aishi Manula kila mara kwa mashambulizi yake, ni straika mzuri, mwenye nguvu ya kushindana na mabeki, mzuri wa mipira ya juu na hata mipira ya chini.

“Kwa muda mfupi niliomfuatilia anaonekana ni mchezaji anayeweza kucheza kokote na kama itatokea nafasi ya kusajili straika, Yacouba atakuwa wa kwanza kwangu, kwani anaonekana ni mtu wa kazi akiwa uwanjani,” alisema kocha.

Aussems alisema anatarajia kutenga muda zaidi wa kumfuatilia kwani anaamini ana vitu vingi vya ziada, ili ikiwezekana aje kuichezea Simba ili mradi akiwa bado akiinoa timu hiyo.

“Ni mapema sana kuzungumza mambo ya usajili wake, ila namfuatilia kuna vitu vilivyonivutia kwake, ila kwa vile nina kazi mbele yangu kuhakikisha Simba inafanya vizuri katika mashindano yaliyo mbele yetu. Ngoja tuone inakuwaje,” alisema.

Katika mechi ya juzi Songne alikuwa msumbufu hasa kwa safu ya ulinzi ya Simba kwani aliwasumbua mabeki Erasto Nyoni, Pascal Wawa na James Kotei ambao walipata wakati mgumu kumzuia.

Songne Yacouba alizaliwa Januari 10, 1992 anaichezea Kotoko kwa mara ya kwanza baada ya kusaini mkataba Januari mwaka huu na mkataba huo utafikia tamati Juni 20, 2021, kitu ambacho kinaweza kuipa kazi Simba kutoboka ili kuvunja mkataba wa straika huyo wa zamani wa Stade Malien.

ISHU YA NDUDA, MSEJA

Makipa wawili wa Simba, Said Mohammed ‘Nduda’ na Emmanuel Mseja juzi Jumatano hawakutajwa kwenye orodha ya kikosi kilichotambulishwa Uwanja wa Taifa, lakini mabosi wa Simba wamedai ni mali yao.

Kaimu Rais wa Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema nyota hao wapo katika orodha ya wachezaji waliowasajili msimu huu, lakini walishindwa kufika uwanjani kwa sababu zao mbalimbali.

“Wapo katika usajili wetu kwani walikosa timu za kwenda mpaka dirisha la usajili lilipofungwa, lakini si hao tu bali hata Haruna Niyonzima, Juuko Murshid nao ni miongoni mwa wachezaji wetu,” alisema.

Lakini Mseja alisema: “Sielewi kinachoendelea, hatujakubaliana kuachana, lakini mpaka sasa sijaambiwa siku ya kuripoti kambini.”