Rashford apewa mikoba ya penalti Manchester United

Muktasari:

Kocha Ole Gunnar Solskjaer amesema kuanzia sasa mshambuliaji Marcus Rashford ndiye atakuwa mpigaji penalti namba moja Manchester United.

London, England. Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amemteua Marcus Rashford kuwa mpigaji penalti namba moja katika kikosi hicho.

Rashford amechukua jukumu hilo ambalo awali lilikuwa chini ya Paul Pogba ambaye siku chache zilizopita aliwakera mashabiki wa Man United kwa kukosa penalti.

Kauli ya Solskjaer imekuja muda mfupi baada ya Pogba kukosa kiki ya penalti katika mchezo wa Ligi Kuu England ambao pengine ingeshinda dhidi ya Wolves. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Rashford alipiga mkwaju wa penalti katika mechi walioshinda mabao 4-0 dhidi ya Chelsea kabla ya Pogba kukosa.

Kitendo cha mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa kukosa penalti kiliibua mjadala kila kona ambapo baadhi ya wachambuzi walimponda.

Mchambuzi wa soka na nguli wa zamani wa Man United, Gary Neville alihoji uongozi wa klabu hiyo kumpa jukumu Pogba kupiga penalti.

Ndani ya miezi 12, Pogba amekosa penalti nne zinazompa sifa ya kuwa mpigaji penalti hodari.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, Solskjaer amewaeleza wachezaji wake kwamba Rashford ndiye atakuwa mpiga penalti namba moja.

Kipa wa Wolves Rui Patricio, aliokoa penalti ya Pogba baada ya kupigwa kwanja na beki Conor Coady ndani ya eneo la hatari.