Rage: Ishu Morrison dakika 10 tu

Wednesday August 12 2020

 

By Imani Makongoro na Oliver Albert

Dar es Salaam. WAKATI sakata la Bernard Morrison na Yanga likipigwa kalenda kwa siku ya pili mfululizo, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF), Ismail Aden Rage ameshangazwa na ucheleweshwaji huo.

Morrison ambaye ni raia wa Ghana, ameingia katika malumbano na Yanga ambayo inadai ni mchezaji wao na ana mkataba wa miaka miwili, ingawa mwenyewe amekanusha akidai hana mkataba nao na hivi karibuni amejiunga na Simba.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Elias Mwanjala alisema sakata hilo litatolea uamuzi Agosti 10 saa 7:00 mchana kabla ya kupigwa kalenda hadi Agosti 11 saa 8:00 mchana, bila mafanikio.

Kwa sasa suala hilo limepigwa kalenda hadi leo. Lakini jana jioni, Rage aliiambia Mwananchi kwamba haoni sababu ya TFF kushindwa kumaliza suala hilo kama taarifa za usajili wa Morrison ziko kwenye TMS.

“Inawezekana mkataba ulioingizwa kwenye TMS ni wa miezi sita, hicho ndicho kinawapa tatizo TFF na Morrison anaendelea kuwatesa Yanga, vinginevyo sioni sababu ya kuchelewesha kutoa majibu ya ukweli wa suala hili,” alisema Rage.

Alisema suala la Morrison kama nyaraka zipo, ni suala ambalo halimalizi dakika 10 kujua ukweli ni upi. Rage alieleza kuwa kama Yanga ilimuongezea Morrison mkataba mpya kabla ya dirisha la usajili wa TFF basi sio halali kwani, hautambuliki kwenye TMS.

Advertisement

MWANJALA: MAMBO NI 50 KWA 50

Baada ya kikao cha jana, Mwanjala aliwaambia waandishi wa habari kwamba, mpaka sasa asilimia ni 50 kwa 50 kwa kila upande katika sakata hilo la Mghana huyo.

Baada ya kikao kirefu cha siku nzima jana kilimalizika saa 10:00 jioni na kisha saa 10:30 Mwanjala alijitokeza kuzungumza na wanahabari ambao, walikuwa wamepiga kambi kwenye ofisi hizo muda wote.

“Tumechukua muda mrefu katika kusikiliza jambo hili, lakini bado tumeshindwa kumaliza kwa sababu kuna nyaraka hazipo.

Tunatarajia nyaraka hizo kutoka Yanga na Morrison mwenyewe itapatika leo jioni kwani wametuhakikishia hivyo na mpaka saa mbili asubuhi kesho (leo) tutakuwa tumeipata.

“Tukishaipata nyaraka hiyo, saa nne asubuhi tutaendelea na kikao na natumaini hadi mchana tutakuwa tumemaliza na kutangaza uamuzi,” alisema Mwanjala.

Alipoulizwa je katika vikao hivyo vinavyoendelea mambo yakoje kwa pande husika alisema: “Iko 50 kwa 50 kila upande hivyo ngoja tuone kesho (leo).” Morrison alitua Yanga katika dirisha dogo la Januari kwa mkataba wa miezi sita kisha ikadaiwa kuwa ameongeza wa miaka miwili.

Advertisement