Rabin Sanya sasa amkuna Milambo

MAPOKEO ya mafunzo sambamba na kipaji alichonacho nyota chipukizi wa soka nchini Rabbin Sanya yameonekana kumkosha Kocha Mkuu wa kikosi cha Vijana U17, Serengeti Boys Oscar Milambo.

Sanya aliyechipukia kupitia michuano ya Ndondo Cup Academy 2018 kwa kuibuka Mchezaji Bora na kupata zawadi ya kwenda nchini Uturuki kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya katika academy ya Besiktas, alijikuta akipata bahati ya kujiunga na timu ya Serengeti Boys kutokana na kiwango cha hali ya juu cha kusakata kabumbu alichokionesha huko.

Uwezo huo ulioonekana na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Ammy Ninje na kumuita nchini haraka kutoka Uturuki kuja kujiunga na Serengeti Boys, imeonekana Sanya alikuwa chaguzi sahihi kuwepo hapo.

Milambo alisema ingawa Sanya bado hajawa ngazi moja na wengine, lakini anayo mapokeo makubwa ya mafunzo anayoyapata kambini, ambapo kipaji chake kikubwa cha kulicheza soka linaonekana wazi wazi.

“Sio rahisi kwa mtu anaekuja kwenye timu kwa mara ya kwanza na kukutana na wachezaji ambao wamekaa kambini zaidi ya mika miwili na kuwa nao sawa kwani watakuwa wamemzidi kitu na hawawezi kuwa kwenye ngazi moja ya mafunzo, lakini kwa yeye amekuwa anapokea mafunzo kwa haraka na ameonesha uwezo na kipaji cha hali ya juu,” alisema Milambo.

“Tunaamini kabisa kama tutaendelea naye na tukafanya mazoezi pamoja kama haya atakuwa mchezaji bora na mwenye kiwango cha juu sana kwenye viwango vya soka kimataifa hivyo ajitahidi kuwa na kasi ya kupokea zaidi na ashirikiane na wengine ili kuwa kitu kimoja na tunufaike na kile alichonacho kama timu na Taifa kwa ujumla,” alisema.

Serengeti iko jijini hapa kwa kambi ya muda mfupi kabla ya kuelekea nchini Uturuki katika mashindano ya UEFA Assist waliyoalikwa na pia maandalizi ya fainali za mataifa ya Africa kwa vijana yatakayofanyika Aprili mwaka huu jijini Dar es Saalam.