Papaa Molinga lazima umpende tu!

NAMBA siku zote huwa hazidanganyi. Wale waliokuwa wakimbeza na kumcheka David Molinga ‘Falcao’ a.k.a Ndama mara alipoletwa nchini na Kocha Mwinyi Zahera kwa sasa wanajisikia aibu!

Kwa wanaokumbuka wakati kocha huyo ambaye alifurushwa Jangwani, mwishoni mwa mwaka jana baada ya chama hilo kuchechemea kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, aliondoka akitoa ahadi ambayo nayo ilibezwa sana hapo awali.

Kocha huyo kutoka DR Congo, alikaririwa akidai kuwa, Molinga angefunga mabao zaidi ya 15 na kama asingefikisha hivyo alikuwa tayari kukatwa mkono ama kulipa fidia ya Dola 1,000 ambayo ni zaidi ya Sh.2 Milioni.

Zahera aliitoa ahadi hiyo baada ya mashabiki kumlaumu kwa kumleta Molinga akitajwa ndiye mrithi wa kuziba nafasi ya Heritier Makambo aliyekuwa ameuzwa AC Horoya ya Guinea.

Hata hivyo, mpaka Ligi Kuu inasimama kutokana na janga la virusi vya corona, tayari Molinga alishawathibitishia mashabiki kwamba yeye ni moja ya washambuliaji mahiri na kama sio kukosa nafasi ya kucheza kwa baadhi ya mechi huenda angekuwa akimbana mbavu Meddie Kagere wa Simba.

MTU HATARI

Kipindi akijiunga na Yanga, Molinga alikuwa kipande flani cha mtu, yaani mutu ya kilo, kwani alikuwa amenene-pa kiasi kwamba ilikuwa ngumu hata kugeuka wakati wa kutaka kuumiliki mpira.

Hata hivyo, baadaye jamaa alirejea kwenye ufiti wake uliopambwa sana na maneno ya Papaa Zahera na kweli jamaa akaanza mambo.

Moto wake ulianzia kwenye mechi za kirafiki za Yanga zilizochezwa Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kujiandaa na mechi zao za kimataifa, walipokuwa wakishiriki michuano la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alianza kwa kuitungua Pamba FC katika mechi iliyopigwa Septemba 7 akiisawazishia bao Yanga jioni kabisa na kufanya matokeo kuwa 1-1, kisha kuja kuzamisha mabao mawili wakati wakiwalaza njaa, Toto Africans kwa mabao 3-0 katika mechi ya Septemba 10.

MKALI WA VICHWA

Mabao yake dhidi ya Toto Molinga alithibishia kuwa yeye ni mkali wa vichwa, kwani alifunga la kwanza kwa kichwa cha kuchupia kabla ya kutupia jingine na kumfanya apate kauli mbele ya vyombo vya habari na hata kumpa maneno Kocha Zahera.

Ligi ilipoanza akadhihirisha kwamba kule jijini Mwanza hakubahatisha, Polisi wakiwa mbele kwa mabao 3-1 alianza kuyapunguza kwa kufunga bao lake la kwanza katika ligi hiyo kwa kichwa cha kuchupia kabla ya kumaliza mchezo kwa bao tamu la ‘frii-kiki’ ya kiufundi iliyoenda moja kwa moja wavuni na kufanya matokeo kuwa sare ya 3-3.

Bao hilo la ‘frii-kiki’ lilizima kebehi alizokutana nazo alipopiga frii-kiki yake ya kwanza alipotua Yanga ambayo aliipaisha juu baada ya kujiandaa kuipiga kwa mikogo mingi kama ya Cristiano Ronaldo.

Bao jingine la kichwa alikuja kuliweka kimiani dhidi ya Ruvu Shooting ‘Wazee wa Kupapasa’ likiisaidia Yanga kulipa kisasi cha kupoteza kwenye mechi yao ya ufunguzi wa msimu huu walipochapwa bao 1-0.

AKILI YA MPIRA

Licha ya kuwa na mwili mkubwa, lakini namna anavyojipanga kwenye lango la adui na jinsi ya kumiliki mpira inadhihirisha wazi kwamba, Molinga ni fundi na mwenye akili ya soka.

Aina yake ya uchezaji ni ile ya washambuliaji walio makini na kazi ya kufunga tu, hana makeke mengi ya kupiga chenga sana ama mbwembwe nyingine, ukiangalia mabao yake dhidi ya Alliance, Singida United na lile la pekee mbele ya Mtibwa Sugar ni uthibitisho wa hilo.

Molinga alifunga mabao hayo kwa utulivu wa akili mbele ya lango la adui. Mbao aliwafunga kwa penalti akithibitisha yuko fiti nyanja zote. Mabao ya kichwa, mabao miguu, frii-kiki na penalti, kote amethibitisha yuko vizuri. Unataka nini zaidi?

KINARA JANGWANI

Kama ulikuwa unamchukulia poa straika huyo kutoka DR Congo utachekwa kwani, ndani ya Yanga yeye ndiye kinara wa mabao akiifungia kwenye Ligi mabao nane, huku katika Kombe la FA ana moja ukiachana na yale ya mechi za kirafiki.

Ndio maana ilishangaza kidogo baada ya kuzagaa taarifa kwamba, straika huyo alikuwa mbioni kutemwa kwenye dirisha dogo ili kuleta mashine nyingine, wakati yeye ndiye anayeongoza kwa mabao na akiisaidia Yanga kuwa kwenye nafasi ya tatu kwa sasa ikiwa na pointi 51.

MWENYEWE FRESHI

Katika mahojiano ya hivi karibuni, Molinga alisisitiza kuwa kazi yake ni kufunga na angependa kupata nafasi nyingi za kucheza kutimiza kile kilichomleta Jangwani, akidai wale waliodhani alikuwa akibebwa na Zahera walikosea kwani alitua Yanga akiwa hatuko fiti.

“Nilikuwa sijacheza kwa muda mrefu wakati nakuja na ujue nilichelewa kambi ya maandalizi, lakini Kocha Zahera alinipa programu kupunguza uzito na kujiweka fiti ndio maana nikarejea kwenye makali yangu ya kufunga. Kazi yangu ni kufunga mabao na si vinginevyo.”

Kabla ya kujiunga Yanga alikuwa akishika nafasi ya tano ya Ufungaji wa DR Congo akitupia 11 FC Lupopo na jumla ya mabao yote ilikuwa 14.