PSG waitaka ugomvi Man U kisa Herrera

Muktasari:

Kumpoteza Herrera litakuwa pigo kubwa kwa Solskjaer, ambaye anapambana kwa nguvu zote kumbakiza mchezaji huyo kama alivyofanya kwa Anthony Martial, ambaye akili yake ilikuwa kuachana na timu hiyo katika kipindi cha Kocha Jose Mourinho.

PARIS Saint-Germain inataka ugomvi na Manchester United baada ya kupanga kuvamia huko Old Trafford kwenda kumng’oa kiungo Ander Herrera.

Kinachoelezwa ni kwamba kiungo huyo wa Kihispaniola amekuwa kwenye mazungumzo na miamba hiyo ya Ufaransa na huenda akajiunga nayo bure kabisa mwishoni mwa msimu huu kama Man United itafeli kwenye mpango wake wa kumsainisha mkataba mpya.

Herrera, atakuwa hana mkataba na Man United mwishoni mwa msimu huu kama hatasaini dili jipya, lakini wabeba hao wa England wanataka staa wao abaki Old Trafford baada ya kuwa kwenye mipango ya Kocha Ole Gunnar Solskjaer. PSG inakoleza moto wake wa kumtaka kiungo huyo ikimpa ahadi ya kumsainisha mkataba unaoanzia miaka mitatu na mshahara wa Pauni 150,000 kwa wiki. Man United ilimnasa Herrera miaka mitano iliyopita akitokea Athletic Bilbao kwa ada ya Pauni 29 milioni. Kumpoteza Herrera litakuwa pigo kubwa kwa Solskjaer, ambaye anapambana kwa nguvu zote kumbakiza mchezaji huyo kama alivyofanya kwa Anthony Martial, ambaye akili yake ilikuwa kuachana na timu hiyo katika kipindi cha Kocha Jose Mourinho.