Ozil kutimkia Marekani, Uturuki

London, England. MESUT Ozil ni bonge la fundi wa mpira na analipwa mshahara mkubwa kuliko wachezaji wote ndani ya kikosi cha Arsenal, lakini hana furaha unaambiwa.

Kwa muda mrefu sasa Ozil amekuwa gumzo huku akika benchi na kelele za kuuzwa zikivuma kila kona ila mwenyewe anataka kumaliza kwanza mkataba wake unaomfanya kulipwa pauni 350,000 kwa wiki ndio asepe zake.

Hata hivyo, habari zinasema kuwa Ozil ataachana na washika bunduki hao wa Emirates msimu ujao wakati mkataba wake utakapofikia tamati na atakwenda kukipiga Ligi Kuu ya Marekani au Uturuki.

Tangu kurejea kwa Ligi Kuu England, Kocha Mikel Arteta hajamchezesha Ozil hata mchezo mmoja licha ya kukaa kwenye benchi katika mechi tatu zilizopita.

Kwa mujibu wa The Sun, kwa sasa Ozil hana mpango wa kuachana na Arsenal kwenye dirisha lijalo la uhamisho na anataka kumaliza mkataba wake ili aondoke akiwa mchezaji huru baada ya msimu ujao.

Uhusiano wa Ozil na mabosi wa Arsenal umezidi kudorora na mara kadhaa wamejaribu kutaka kumuuza lakini, mwenyewe amegoma na kuendelea kubaki Emirates kwa msimu mpya wa 2020-21.

Hatua ya Ozil, 31, kuamua kuwa akimalizana na Arsenal atakwenda kukipiga Marekani au Ligi ya Uturuki ambako ana uhusiano wa karibu na Rais wa nchi hiyo Recep Erdogan, ni kukwepa kurejea Bundesliga kutokana na kukosolewa vikali nchini mwake.

Imeripotiwa kuwa Ozil amewaambia marafiki zake kwamba, anafikiria kuwa atakwenda kuonyesha makali yake kwenye ligi hizo mbili maarufu duniani.