Ole noma, Sancho, Havertz anabeba

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer ameripotiwa kushika usukani kwenye mbio za kufukuzia huduma ya staa moto kabisa kwenye soka la Ujerumani kwa sasa, Kai Havertz.

Man United wanamtazama staa huyo wa Bayer Leverkusen kuwa ni mwenye kipaji cha kutosha cha kwenda kucheza kwenye kikosi chao wakiamini kwamba atakuwa mchezaji wa daraja la juu sana siku chache zijazo.

Kocha Solskjaer amepanga kuua ndege wawili kwa mpigo huko Ujerumani, akimtaka pia staa wa Borussia Dortmund, Jadon Sancho, ambaye usiku wa juzi Jumapili alipiga hat-trick, wakati timu yake ilipoichapa Paderborn 6-1 kwenye Bundesliga.

Mpango namba moja ni kumsajili Sancho, lakini baada ya hapo watamnasa pia Havertz, ambaye wanaamini wasipofanya hivyo mwaka huu basi thamani yake itakuwa kubwa zaidi mwakani.

Kwa kuanzia, Man United imepeleka ofa ya Pauni 50 milioni ya kunasa saini ya Havertz, huku wakiamini mkwanja huo utatosha kabisa kwenye kupata huduma ya mchezaji huyo wanayemsaka kwa nguvu zote.

Havertz amekuwa akiwindwa na vigogo msimu huu baada ya kufunga mabao 15 katika michuano yote. Man United wameshafahamu watamtumiaje, ikiwa ni pamoja na kumchezesha kwenye wingi moja au akitokea kwenye kiungo ya kati.

Mpango ni kwamba Havertz atacheza kulia, kushoto atakuwapo Sancho na Marcus Rashford atasimama katikati. Hata hivyo, huduma ya Sancho haiwezi kupatikana kirahisi, lazima mkwanja unaoanzia Pauni 100 milioni na kuendelea.

Aidha, United imekubaliana na klabu ya Shanghai Shenhua ya China kubaki na Odion Ighalo hadi Januari 2021.