Ole afyeka 15, Mata abaki

Muktasari:

Licha ya kwamba hatakuwa akianzishwa katika kila mechi, lakini nyota huyo wa zamani wa Chelsea anabaki kuwa mmoja wa wachezaji wenye vipaji vya asili waliopo kwenye timu hiyo.

MANCHESTER, ENGLAND.FAGIO linapita huko Manchester United huku kocha Ole Gunnar Solskjaer ameamua kumpa mkataba mpya kiungo wake wa Kihispaniola, Juan Mata.
Mkataba wa sasa wa Mata utafika tamati mwishoni mwa mwezi huu na kwamba atakuwa huru kuondoka kwenye timu hiyo bure kabisa kama kutakuwa na timu itahitaji saini yake. Lakini, Man United wamethibitisha kwamba wamempa ofa ya mkataba mpya staa huyo mwenye umri wa miaka 31 wakiamini kwamba bado kuna kitu atakifanya chini ya kocha Solskjaer.
Bosi huyo wa Man United, Solskjaer ameamua kuwafunguliwa mlango wa kutokea wachezaji 15 kutokana na mikataba yao kufika mwisho na miongoni mwao wapo mastaa, Ander Herrera na Antonio Valencia.
Kinda aliyeibukia kwa kasi sana na kupotea James Wilson naye yupo kwenye orodha hiyo ya wakali walioonyeshwa mlango wa kutokea Old Trafford. Kitendo cha kumbakiza Mata kinamfanya kocha huyo kuamini kwamba kiungo huyo mchezeshaji bado yupo kwenye mipango yake kwa ajili ya msimu ujao.
Licha ya kwamba hatakuwa akianzishwa katika kila mechi, lakini nyota huyo wa zamani wa Chelsea anabaki kuwa mmoja wa wachezaji wenye vipaji vya asili waliopo kwenye timu hiyo. Nidhamu yake ya uwanjani ndicho kitu kinachomfanya kocha Solskjaer kumtaka aendelee kubaki kwenye vyumba vya kubadilishia vya klabu hiyo. Hata mshahara anaotaka kulipwa si ule wa kuvunja benki ambao uliwafanya washindwe kwenye kumbakiza Herrera na kwamba Mata atapewa mkataba wa miaka miwili.
Wachezaji ambao wanatemwa na Man United ni pamoja na Herrera, Valencia, Regan Poole, Zak Dearnley, Tom Sang, Callum Whelan, Matty Willock, James Wilson, Matthew Olosunde, Tyrell Warren, DJ Buffonge, Callum Gribbin, Josh, Baars Bohui na James Thompson.