Kagere, Okwi ni battle

Sunday May 10 2020

 

By CHARLES ABEL

KASI ya kupachika mabao ya Meddie Kagere imemfanya awe kipenzi cha mashabiki na wanachama wa Simba tangu alipojiunga nayo mwaka 2018.

Kagere amefunga jumla ya mabao 42 katika Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili tofauti na katika Ligi ya Mabingwa Afrika amepachika mabao saba (7) huku pia akipachika mabao matano (5) katika Kombe la Kagame akiwa na Simba.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo aliyopata ndani ya muda mfupi, Kagere ana mtihani wa kufikia au kuvuka mafanikio ya nyota mwingine aliyepita ndani ya klabu hiyo, Emmanuel Okwi. Anapaswa kuhenya kwelikweli. Okwi, ambaye kwa sasa anaichezea Al Ittihad ya Misri, amefanikiwa vilivyo ndani ya Simba katika nyakati tofauti alizoichezea tangu alipojiunga nayo kwa mara ya kwanza mwaka 2009 akitokea SC Villa ya Uganda.

Nakupa tathmini ya mafanikio kadhaa ambayo Okwi ameyapata ndani ya Simba yanayompa changamoto kubwa Kagere ya kuhakikisha anayafikia au kuyavuka ndani ya timu hiyo.

MATAJI LUKUKI

Kagere ametwaa taji moja tu akiwa na Simba ambalo ni la Ligi Kuu msimu uliopita na upo uwezekano wa kutwaa la pili ikiwa timu hiyo italitetea taji hilo msimu huu ambapo, ina uwezekano mkubwa kufanya hivyo.

Advertisement

Hali ni tofauti kwa Okwi, ambaye mataji ya Ligi Kuu pekee ametwaa mara nne akiwa na Simba ambapo, ni katika msimu wa 2009/2010, 2011/2012, 2017/2018 na 2018/2019.

Kana kwamba haitoshi, Okwi ameshinda taji moja la Kombe la Mapinduzi akiwa na Simba na pia mataji matatu ya ngao ya jamii.

FUNDI WA DABI

Sio kazi rahisi kwa wachezaji kufunga mabao mara kwa mara katika mechi zinazohusisha watani wa jadi, Yanga na Simba lakini kwa Okwi hadithi ni tofauti.

Raia huyo wa Uganda ni miongoni mwa nyota waliofunga idadi kubwa ya mabao katika mechi za watani wa jadi ambapo, amepachika jumla ya mabao manne. Matatu ameyafunga kwa nyakati tofauti alipokuwa akiichezea Simba na moja lingine alifunga pindi alipokuwa akiitumikia Yanga.

Hili ni deni lingine kwa Kagere analopaswa kulilipa kwa Okwi kwani, yeye amefunga mabao mawili tu katika mechi zote za Simba dhidi ya Yanga ambazo amecheza tangu alipotua nchini mwaka 2018.

BILA KUFUNGWA

Kuchukua ubingwa huku timu ikiwa imeweka rekodi fulani ya kipekee ni jambo la aina yake na ambalo kila mwanasoka duniani analitamani.

Moja ya rekodi hizo ni ile ya kutwaa ubingwa huku timu ikiwa haijapoteza hata mechi moja kama walivyofanya Simba katika msimu wa 2009/2010.

Ndani ya misimu miwili ambayo Kagere ameichezea Simba, timu hiyo imeshindwa kufanya hilo ingawa inaweza kulitimiza msimu ujao japo sio jambo rahisi.

KIMATAIFA

Katika mashindano ya klabu Afrika, Kagere ameifungia Simba mabao saba tu ikiwa ni kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu wa 2018/2019 ambao pia alishika nafasi ya pili kwa ufungaji katika mashindano hayo.

Lakini bado pamoja na kufanya kazi hiyo nzuri, ana kibarua cha kupindua rekodi ya Okwi ambaye katika mashindano ya klabu Afrika amefunga jumla ya mabao 10 ambapo, tisa (9) amepachika akiwa anaitumikia Simba na moja amefunga wakati alipokuwa Yanga.

Mbali na hilo, Kagere katika kipindi chote alichoi chezea Simba, amefunga bao moja tu ugenini katika mechi za kimataifa ambapo ilikuwa ni pale timu hiyo ilipoibuka na ushindi wa mabao 4-0 ugenini dhidi ya Mbabane Swallows.

Hata hivyo, ni tofauti na Okwi ambaye amepachika jumla ya mabao manne ugenini ambayo ni dhidi ya timu za Mbabane Swallows, ES Setif, Al Ahly, Gendarmarie na TP Mazembe.

HAPA NGOMA DROO

Wawili hao kila mmoja amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara ambapo, Okwi aliibuka kinara katika msimu wa 2011/2012 wakati Kagere alitwaa msimu uliopita.

KOTEI, AUSSEMS WAWAPA TANO

Kocha wa zamani wa Simba, Patrick Aussems alisema wachezaji hao wote wawili wana umuhimu mkubwa ndani ya uwanja

“Ni wachezaji ambao wanajua majukumu na wajibu wao uwanjani, wana utulivu, wanaweza kufunga mabao na kuzalisha mabao kwa wengine.

Katika wachezaji ambao nimefurahia kufanya nao kazi pamoja Okwi na Kagere ni miongoni mwao,” alisema Aussems.

Kwa upande wake Kotei alisema uwepo wa wachezaji hao uliongeza kitu kikubwa Simba.

“Wana weledi wa hali ya juu na wanaweza kuamua matokeo ya mechi. Unapokuwa nao uwanjani kazi inakuwa sio ngumu,” alisema Kotei.

Advertisement