Nyota wazugaji kukiona Kigoma Sisters

Muktasari:

Kocha wa Kigoma Sisters,Daud Lawrence‘Siang’a’amesema watakaporejea kambini atawapima kwa mazoezi ya nguvu wachezaji wake na wale watakaokuwa fiti ndio watakaoanza kikosi cha kwanza katika Ligi kuu ya Wanawake.

KOCHA wa Kigoma Sisters, Daud Lawrence ‘Siang’a’ amesema watakaporejea kambini atawafanyisha mazoezi ya nguvu nyota wake ili kubaini kama walikuwa wakijifua kwani aliwapa programu maalumu ya kuifuata.
Siang’a alisema wakati wanavunja kambi aliwapa kila mchezaji programu maalumu ya kuifanya atakapokuwa nyumbani kipindi hiki ambacho ligi imesimama kupisha janga la mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona.
Alisema timu itakaporejea atawapima wachezaji wake kwa mazoezi ya nguvu na wale watakaokuwa fiti ndio atawapa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
“Nimewapa programu ya kuifanya kipindi hichi ambacho wapo nyumbani nitakachofanya tukirejea nitawapima na wale watakaokuwa wamezembea nitawagundua tu hivyo wanatakiwa huko walipo wafanye mazoezi ya nguvu,” alisema Siang’a.
Kocha huyo alisema anataka watakaporejea kambini wasianze upya badala yake waendelee na mazoezi ndio maana aliwapa maelekezo ya kufanya wakati huu wapo nyumbani.
Alibainisha wazi kuwa kubwa ambalo linawasumbua kwenye kikosi chake ni wachezaji wake kukosa stamina jambo ambalo atalifanyia kazi  watakaporejea kwa kuwapa mazoezi ya fiziki ili wawe na nguvu ya kutosha.