Nyota 7 Simba Sc fyekelea mbali

WAKATI leo Jumatatu Simba ikitarajiwa kurudi tena kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuonyeshana kazi na Azam FC, imefichuka kwamba kuna mastaa saba wapo mkao wa kufyekelewa mbali. Yaani msimu ujao wa 2019-2020 hawatavaa jezi za Wekundu wa Msimbazi.

Simba ikitoka kupoteza mechi yao ya tatu mbele ya Kagera Sugar, mabosi wake wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed ‘Mo’ Dewji wamekubaliana kukisuka upya kikosi hicho ili kuongeza ushindani msimu ujao.

Katika kuweka mambo sawa, Mo Dewji na viongozi wenzake wamekubaliana kumbakiza kikosini kocha Patrick Aussems, ambaye mkataba wake wa sasa upo ukingoni kwa kumpa mpya wa mwaka mmoja.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imepenyezewa ni kwamba, tayari Aussems amepewa nakala ya mkataba na anachosubiri ni kutua kwa wakala wake aishie nchini Ubelgiji ndipo mambo yakamilike. Mara baada ya kumaliza kazi hiyo, Aussems atawasilisha orodha ya majina ya wachezaji ambao hatakuwa na mipango nao kwa msimu ujao na kuleta mengine ambao atataka wasajiliwe ili kuongeza makali. Hata hivyo, imeelezwa kuwa kuna mastaa saba ambao watafyekelewa mbali ili kutoa nafasi ya kutua majembe mapya klabuni hapo.

Nyota ambao wako hatarini kufyekwa ni pamoja na wale wenye majeraha ya muda mrefu, umri mkubwa hivyo kushindwa kwenda na kasi ya Simba ambayo inalenga kufanya vizuri kimataifa kwa msimu ujao.

Miongoni mwa mastaa hao yupo beki kisiki Pascal Wawa, ambaye alitua bure mwanzoni mwa msimu huu huku sababu ikiwa ni majeraha na umri mkubwa.

Pia wamo Mghana Asante Kwasi na Salim Mbonde, ambaye tangu ameumia msimu uliopita hajarejea uwanjani licha ya kuanza kupona.

Wengine ni Juuko Murshid na Nicholas Gyan ambao wataachwa kutokana na mikataba yao kufikia mwisho huku kukiwa hakuna mpango wa kuwaongezea mkataba mpya. Hata hivyo, mabeki hao wanawindwa na Yanga.

Straika Adam Salamba, ambaye amefunga mabao manne msimu huu, bado ana mkataba na Simba na taarifa zinaeleza kuwa huenda akatolewa kwa mkopo ili kupata uzoefu zaidi huku kipa Deo Munishi ‘Dida’ yuko njiapanda na atafunguliwa mlango kama Simba itasajili kipa mpya huku Beno Kokalanya akitajwa kuwindwa na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara.

MSIKIE MENEJA

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alipoulizwa kuhusiana na kutemwa kwa mastaa hao saba, alisema kwa jinsi ratiba ilivyo imewapa changamoto kufahamu kwa haraka wachezaji ambao, itaachana nao mwishoni mwa msimu huu.

Alisema kuwa awali haikuwapa shida kufahamu wachezaji wa kuwaacha kwani, baadhi walikuwa nje kwa muda mrefu kwa kukosa namba huku wengine wakiwa majeruhi, lakini ratiba ya sasa imebadilika na wengine wanapata nafasi ya kucheza kulingana na mahitaji ya mwalimu.

“Niseme wazi tu, kama kuna mchezaji atakayeondoka Simba ni kwa mahitaji yake mwenyewe labda kuna maslahi makubwa, lakini benchi la ufundi tutahakikisha kila mchezaji muhimu ambaye tunamuhitaji tunabaki naye kikosini.

“Usajili tutafanya kulingana na maeneo yenye mapungufu msimu huu, lakini wachezaji ambao tutasajili ni wale wenye uwezo mkubwa na akifika hapa Simba si wa kumfanyia majaribio tena kama ilivyokuwa hapo awali, anatakiwa kuingia moja kwa moja kwenye mfumo na kuanza kucheza kama atashindwa basi ni mwenyewe tu,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alisema wachezaji wao muhimu wanaomaliza mikataba mwisho wa msimu huu, watapewa mipya na watakisuka upya kikosi chao ili kuwa imara zaidi kulingana na mashindano yote kwa msimu ujao.

“Timu ina malengo yake kwa msimu ujao, lakini kwa sasa tunataka kutetea ubingwa wetu wa ligi kisha tutafanya usajili mzuri kulingana na mahitaji ya kocha, ila kama kocha atataka kuachane na yeyote tutafanya hivyo.”

Leo Jumatatu Simba itakipiga na Azam kwenye mchezo muhimu wa Ligi Kuu Bara huku ikijipanga pia kukipiga na Sevilla ya Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, ikiwa ni mchezo wa kirafiki ulioratibiwa na wadhamini wao, kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa Tanzania. Mchezo huo utapigwa Mei 23, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na tayari mastaa wa Simba akiwemo nahodha John Bocco, wametangaza kuwa watahakikisha wanafanya kweli.

Bocco alisema kuwa, wamejipanga kuitumia vyema fursa hiyo kutangaza vipaji vya soka vilivyopo nchini na kwamba, wanawasubiri kwa hamu wababe hao wa Europa League, watakaotua nchini Mei 21.