Nyoni, Yondani hapana!

Muktasari:

  • Walichokifanya mabeki wa Taifa Stars, Kelvin Yondan na Erasto Nyoni dhidi ya Cape Verd kimewakuna wanasoka wa zamani na kwamba wanastahili kuigwa na chipukizi

BEKI Erasto Nyoni na Kelvin Yondani wameonyesha mfano wa ukongwe wao ndani ya kikosi cha Taifa Stars baada ya kufanya kazi kubwa ya kuwadhibiti washambuliaji wa Cape Verde katika mechi ya marudiano ya juzi ya kuwania kufuzu fainali za Afcon.

Nyota wa zamani walionyeshwa kuguswa na kombinesheni ya wazoefu hao na kuwamwagia sifa, ambapo Sekilojo Chambua alitoa mtazamo wake kuhusiana na wachezaji hao na kombinesheni yao ndani yake ilikuwa na umakini, ujuzi pamoja na uzoefu wa michuano ya kimataifa.

“Walichokifanya Yondani na Nyoni mbele ya washambuliaji wa Cape Verde ambao walikuwa warefu, kimeonyesha namna ambavyo wanastahili kuigwa dhidi ya chipukizi wanaoitwa ndani ya kikosi cha Stars.

“Tofauti na walivyocheza Hassan Kessy na David Mwantika ugenini, sina maana kwamba ni wabaya la, ila Nyoni na Yondani walikuwa wanaziba njia za kupita wapinzani wao,” alisema nyota huyo wa zamani.

Mbali na kuwazungumzia Nyoni na Yondan, pia aligusia penalti aliyopiga Mbwana Samatta kwamba angepatia ingempa krediti kubwa kwa namna alivyouchopu mpira, lakini kwa kuwa alikosea ndio maana mashabiki wana manung’uniko.

“Penalti kama zile asilimia kubwa zinapigwa na wachezaji wa Ulaya ni za kiufundi wa hali ya juu, lakini kwa kuwa amekosea plani zake na ndio maana ilionekana kapiga ovyo.”

Naye Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal ‘Bilo’ alisema Nyoni na Yondani walicheza kwa kiwango cha hali ya juu dhidi ya Cape Verde, akieleza kiufundi kwamba kujiamini kwao kuliwafanya washambuliaji wa upinzani kushindwa kuvuka ngome yao iliyokuwa makini kuondosha rabsha zote.