Nyie Arsenal hebu msikieni Unai Emery

Muktasari:

Emery alipoulizwa kama kikosi chake cha msimu huu kutakuwa bora kuliko cha msimu uliopita, alisema: “Sijui.

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa Arsenal, Unai Emery amedai kwamba hajui kama usajili aliofanya kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi utaboresha kiwango cha kikosi chake au la.
Arsenal wametumia Pauni 138 milioni kunasa wachezaji watano wapya sambamba na dili mnoja la mkopo la kiungo Dani Ceballos kutoka Real Madrid, huku wakiondoa pia wachezaji watano kwenye kikosi na kuingiza Pauni 54 milioni.
Kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England waliocheza na Newcastle United na kushinda 1-0 shukrani kwa bao la Pierre-Emerick Aubameyang, kocha Emery hakumwaanzisha mchezaji wake yeyote mpya, si yule wa pesa nyingi Nicolas Pepe wala beki mwenye uzoefu David Luiz aliyecheza. Lakini, jana kikosi hicho kilikabiliana na Burnley na wakali wapya kadhaa walitazamiwa kucheza mechi hiyo ya Emirates.
Emery alipoulizwa kama kikosi chake cha msimu huu kutakuwa bora kuliko cha msimu uliopita, alisema: “Sijui.
“Mpango wetu ulikuwa kuboresha kuliko tulivyokuwa msimu uliopita, kuboresha mambo yetu, kuboresha ushindani wetu na kufikia malengo, lakini sijui kama hiki ni kikosi bora au la. Nina uhakika, lakini nina machaguo mengi.”
Mesut Ozil na Sead Kolasinac, ambao hawakucheza mechi ya kwanza kutokana na wasiwasi wa kuhusu usalama wao baada ya kuvamilia na majambazi hivi karibuni wameungana na wenzao kwenye kikosi huku kocha Emery akitaka kukiweka sawa kikosi chake kutokana na ukweli kwamba manahodha wake watano wa msimu uliopita, watatu Laurent Koscielny, Petr Cech na Aaron Ramsey wameondoka.