Nkana hawahitaji kiingereza cha Kessy

Muktasari:

  • HASSAN KESSY alicheza vizuri mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa aliwadhibiti vilivyo washambuliaji wa Simba wasiweze kuleta madhara langoni mwa timu yake

HASSAN KESSY alicheza vizuri mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyokutanisha timu yake ya Nkana Red Devils dhidi ya Simba, Jumamosi iliyopita.

Akicheza nafasi ya beki wa kulia kama ilivyo kawaida yake, aliwadhibiti vilivyo washambuliaji wa Simba wasiweze kuleta madhara langoni mwa timu yake kwenye mchezo ule ambao walikuwa nyumbani pale jijini Kitwe.

Hakuishia kwenye kulinda tu, Kessy alipandisha mashambulizi mara kwa mara na kumimina krosi nyingi ambazo iwapo zingetumiwa vizuri na washambuliaji wa Nkana, pengine wangeimaliza mechi kulekule kwao.

Siku moja baada ya mchezo ule kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kessy aliandika ujumbe fulani kwa lugha ya Kiingereza akionyesha hana bifu na kiungo wa Simba, Jonas Mkude ambaye kuna nyakati katika mchezo huo walikwaruzana.

Niliupenda ujumbe wa Kessy na kuuelewa vizuri. Wala hakukuhitajika elimu ya kiwango cha juu kuelewa nini alikilenga licha ya ujumbe wake kuandikwa kwa Kiingereza ambacho hakikuwa kimekamilika.

Niliwaza baada ya kiwango kile bora ambacho Kessy alikionyesha kwenye mchezo ule wa kwanza baina ya Simba na Nkana, mijadala mingi ingehusu namna beki huyo alivyoimarika tangu alipoanza kucheza soka la kulipwa pale Zambia.

Kabla hajaondoka nchini kwenda Zambia, Kessy alikuwa na mapungufu mengi ya kiufundi ndani ya uwanja ambayo kwa namna moja ama nyingine yalikuwa yanamgharimu yeye na timu alizokuwa anazichezea kuanzia Mtibwa, Simba hadi Yanga.

Nkana imeonekana kumbadilisha Kessy kwani kabla hajajiunga nayo, alikuwa anashindwa kuwa na uwiano mzuri wa kuzuia na kushambulia kama ambavyo amekuwa akifanya hivi sasa kwenye timu hiyo ya Zambia.

Ameongeza utulivu, umakini na hata kiwango chake cha nidhamu ndani ya uwanja kimeimarika kwa kiasi kikubwa tofauti na hapo kabla ambapo alikuwa akifanya faulo za kijinga ambazo zilimfanya aishie kuonyeshwa kadi ama za njano au nyekundu.

Hata hivyo, tofauti na matarajio yangu, badala ya wengi kujadili mabadiliko makubwa kiufundi ambayo Kessy amekuwa nayo, mjadala juu ya beki huyo umeonekana kulenga zaidi Kiingereza alichotumia kuandika ujumbe wa kuonyesha hana ugomvi na Mkude.

Kessy huyu ambaye leo watu tunatumia muda mwingi kukosoa uwezo wake wa kuandika lugha ya watu, tunasahau kuwa alifanyia kazi kwa vitendo kilio cha muda mrefu cha Watanzania wenye kiu ya kutaka kuona wachezaji wao wanatoka kwa wingi kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa.

Kumkosoa kwa mambo ambayo hayana msingi, mchezaji kama Kessy ambaye ameonyesha uthubutu wa kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa ni kutomtendea haki kwani kilichompeleka Zambia ni kipaji chake na sio uwezo wa kuzungumza au kuandika Lugha ya Kiingereza.

Bado Tanzania ina kundi kubwa la wachezaji wanaocheza ligi ya ndani ambao tunahitaji kuwaona wanafuata nyayo za kina Kessy, kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa badala ya kuendelea kubakia hapa nchini.

Wanahitaji kuaminishwa kuwa lugha sio kigezo kikuu cha wao kupata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania na badala yake ni vipaji vyao uwanjani.

Tukumbuke wengi wao hawakupata nafasi ya kutosha kujifunza lugha lakini pia Kiingereza sio lugha ya asili ya Watanzania, hivyo wanapoona ukosoaji wa mwenzao wanakata tamaa ya kujaribu kwa hofu ya kukutana na ukosoaji kama uliomkuta Kessy.

Lakini pamoja na hilo, Kessy alipaswa kutazamwa kama shujaa na mfano bora kwa wengine kwani ameonyesha uthubutu wa hali ya juu na kujiamini, roho ambayo itamfanya apige hatua kubwa siku za usoni.

Alianza kuthubutu kwa kuachana na soka la kutegemea Simba na Yanga hapa nyumbani na kwenda kutafuta maisha nchi za watu akafanikiwa lakini sasa anaonyesha uthubutu wa kutumia lugha ambayo sio asili yake.

Ipo mifano ya kundi kubwa la wachezaji ambao wanafanya vizuri kwenye soka duniani pasipo hata kufahamu kiingereza cha kuombea maji na mfano ni mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi ambaye anazungumza Kihispania lakini hilo halimzuii kung’ara.

Ondoa Messi, kuna Carlos Tevez ambaye alicheza kwa mafanikio Manchester United, Manchester City na West Ham lakini hadi anaondoka England bado alikuwa hajamudu kuandika wala kuzungumza Lugha ya Kiingereza.

Badala ya kumkosoa Kessy kwa kukosea kuandika Kiingereza ni vizuri watu wangetumia nafasi hiyo kumkosoa kwa makosa ya kiufundi anayoonyesha ili ayafanyie kazi na aweze kufika mbali zaidi.

Tunapaswa kumhukumu Kessy kwa mapungufu ya kisoka aliyonayo kwa sababu mwisho wa siku, Nkana na timu yoyote ile nje ya nchi, itampima kwa ufanisi wake ndani ya uwanja na sio uwezo au udhaifu wa kuzungumza na kuandika Kiingereza.