Niyonzima: Nisingerudi Yanga wala nisingekuwa na amani

UKIANZA kutaja viungo bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara basi huwezi kuacha kulitaja jina la Haruna Niyonzima kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira na anavyojua kuuchezea.

Haruna amaecheza nchini Tanzania kwa mafanikio katika klabu ya Yanga na Simba kisha akaondoka nchini kwenda kwao kukipiga As Kigali ambapo alicheza kwa muda mfupi tu kisha akarejea Yanga na kusaini mkataba wa miaka miwili.

Mwanaspoti lilimtafuta kutaka kufahamu undani wa yeye kurejea nchini ikiwa tayari alikuwa ameshaanza maisha yake mapya akiwa nyumbani kwao Rwanda.

HAKUWA NA AMANI KUIACHA YANGA

Niyonzima baada ya kumaliza mkataba wake na kuondoka nchini, anasema moyoni mwake alikuwa hajisikii vizuri lakini hakuwa na jinsi ila kuanza maisha mengine mapya.

Na ilipotokea ofa ya kurejea Yanga aliona ni wakati sahihi kurejea ili aweze kuwaaga vizuri mashabiki zake kutokana na kuishi nao vizuri.

“Ofa zilikuwepo nyingi lakini mimi binafsi nilitaka kurudi Yanga, nilitoka Yanga kwa amani na nilipata mafanikio mengi nikiwa na Yanga kwahiyo nikaona bora nirudi Yanga ili nikiondoka basi moyo wangu uwe na amani, sikutaka niondoke nikiwa nasemwa semwa maana kusemana na watu haipendezi na hapa nilipo nina amani ya moyo.”

APATA KIGUGUMIZI, SIMBA NA YANGA

Wachezaji wengi huwa wanazungumza utofauti wa timu ambazo wamepitia lakini upande wa Niyonzima imekuwa ni tofauti.

Niyonzima ambaye amecheza Simba na Yanga kwa nyakati tofauti alibaki mdomo wazi kuelezea tofauti za klabu hizo.

“Dah kaka inatosha kusema utofauti upo, utofauti hata kwenye jezi hapa njano kule nyekundu nikisema hivyo inatosha.”

ATUKANWA, ASEMWA KISA KWENDA SIMBA

Baada ya kuachana na Yanga ambayo alikaa takribani miaka sita (2011-2017), Niyonzima aliamua kuondoka Yanga na kujiunga na Simba ambayo alikaa kwa miaka miwili (2017-2019).

Akiwa na Simba, alipata majaribu mengi kutoka kwa mashabiki wa Yanga lakini hakukata tamaa.

“Changamoto zilikuwepo lakini mengi ni yale yale, nilitukanwa sana lakini nilikuwa nachukulia kama maisha ya mpira tu yanapita,”.

“Wapo ambao ni mashabiki wa Yanga na nilikuwa nakaa nao na kupiga nao stori wanaelewa kwamba ni maisha, lakini wengine ndio hawaelewi.”

AWASIHI WACHEZAJI BONGO KUTOKA

Imekuwa kawaida wachezaji mbalimbali kutoka nchi tofauti kuja Tanzania kucheza soka kisha kuondoka wakiwa wametajirika.

Lakini imekuwa ni changamoto sana kwa wachezaji wengi wa Tanzania kuondoka na kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Niyonzima anawapa somo wachezaji wa Bongo kwamba wasiwe na woga wa kujaribu kwani wakishindwa wanarudi na kujipanga upya.

“Kutoka ni malengo ya mtu binafsi ili kuweza kupata changamoto, hapo unajengeka zaidi na wanabidi watoke ili hata ikishindikana wanarudi kujipanga zaidi na kutoka tena.”

SIRI YA KUDUMU KWENYE SOKA

Umri uliopo kwenye hati ya kusafiria wa kiungo huyu ni kwamba ana miaka 30, sio miaka haba sana lakini bado ameweza kucheza katika kikosi cha kwanza katika kila timu anayoenda.

Niyonzima amezidi kuonekana fundi lakini wengi hawajui ni kitu gani ambacho kinamfanya awe hivyo.

“Kitu cha kwanza nauheshimu sana mpira kwasababu ndio kazi yangu, nafanya sana mazoezi ndugu yangu, yani sina masikhara kwenye upande huo, lakini pia nafata programu zote ambazo huwa napewa,”.

KUIGIZA KWAKE NI KAMA KAWA

Niyonzima anasema kabisa kwamba licha ya kuwa na kipaji cha soka, yeye ni mtu ambaye anapenda sana muziki pamoja na kuigiza.

Katika hilo ameweka wazi kwamba kuna kazi moja imeshamalizika lakini pia anajipanga kufanya kazi nyingi zaidi.

“Mimi binafsi napenda sana kuangalia muvi, kusikiliza muziki na kupumzika kutokana na kazi yetu kuhitaji tupate muda wa kupumzika mwingi.

“Filamu napenda na watu wanatakiwa kujua kwamba kuna vitu vingi vinakuja, ile kipande kilichooonekana kimechelewa kutoka kwa sababu ya corona lakini pia kuna projekti nyingi zinakuja watu wataona kipaji changu kingine.”

Anasema muda wa kufanya hivyo upo kutokana na kwamba filamu haitumii muda mwingi na hata mpira pia ndio maana mtu anaweza akawa anasoma huku anacheza mpira.

KUHUSU MKE WA TATU, MH!

Niyonzima mwanzoni mwa Mfungo wa Ramadhan alifunga ndoa na mke wa pili, Mwanaspoti lilimuuliza kama ana mpango wa kuongeza kama ambavyo dini yake inaruhusu.

Niyonzima alisema hapendi kuweka wazi maisha yake binafsi ila kikubwa ambacho anataka ni kuona jambo ambalo analifanya yeye familia yake inafurahia.

“Naruhusiwa kuoa mpaka wanawake wanne, lakini kuoa ni mambo ya siri na kikubwa nafanya kile ambacho familia yangu wanakifurahia.”

MPIRA WAMPA MAISHA

“Nina sehemu zangu za kuishi na watoto wanajivunia wapo kwao, mpira ni kazi na ndio maana nauheshimu.”