Nisameheni nilipagawa tu – Klopp

Muktasari:

  • Bao la dakika za nyongeza lililoipa Liverpool ushindi wa 1-0 dhidi ya mahasimu wao Everton kwenye Uwanja wa Anfield lilimpagawisha kocha Jurgen Klopp na kumfanya afanye kosa kubwa la kuingia uwanjani kushangilia, hata hivyo ameomba radhi kwa kitendo hicho. 

Liverpool, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, amewaomba radhi mashabiki na wadau wa soka kutokana na kitendo chake cha kuingia uwanjani wakati akishangilia bao la dakika za lala salama.

Klopp amesisitiza kuwa alimuomba radhi pia mwamuzi wa mchezo kati yao na mahasimu wao wa jiji la Liverpool ‘Merseyside derby’ timu ya Everton, Chris Kavanagh pamoja na kocha Marco Silva.

“Ninawaomba radhi wote, sio kitu nilichopanga kukifanya lakini imetokea, furaha ya bao ilinichanganya na kujikuta nimeingia uwanjani,” alisema.

Katika mchezo huo ambao ulionekana kama utamalizika kwa sare ya bila mabao, Liverpool ilijipatia bao pekee katika dakika ya mwisho ya mchezo huo baada ya 90 kukamilika na mwamuzi wa akiba kuongeza nne ambapo mtokea benchi Divock Origi alifunga dakika ya 90+05.

Mshambuliaji huyo chipukizi mwenye asili ya Kenya, aliyatumia vema makosa ya kipa wa Everton, Jordan Pickford, aliyeshindwa kuudaka wala kuupangua mpira uliogonga mwamba wa juu kabla ya kumkuta chipukizi huyo aliyeujaza wavuni.

Baada ya kuingia kwa bao hilo lililowaamsha mashabiki wa Liverpool, Klopp alikurupuka kutoka katika eneo lake na kukatiza uwanjani akienda kumpongeza kipa wake Alisson Becker.

“Mara baada ya kuzinduka nilienda kumuomba radhi mwamuzi Chris Kavanagh na baadaye nilimfuata kocha Marco Silva na kumuomba msamaha wote walinielewa ni makosa ya kibinadamu tu,” alisisitiza.

Akiuzungumzia mchezo huo, Klopp alisema ulikuwa mgumu kwa kila upande na akawapongeza Everton kwa kuonyesha uwezo mkubwa na kukiri kwamba aliamini mchezo utamalizika kwa sare.

“Siku zote mchezo wa mahasimu huwa mgumu lakini huu wa leo ‘jana’ ulikuwa mgumu zaidi, ulikuwa na ushindani na ufundi wachezaji wa timu zote walicheza vema lakini ilikuwa ngumu kutengeneza nafasi za kufunga mabao,” alisema.

Klopp alikiri kuwa ushindi wao haukutokana na uwezo bali bahati iliyowawezesha kujipatia bao hilo katika dakika ya 90+05 ambapo zilibaki sekende chache mwamuzi apulize kipenga cha kumaliza mchezo.

Kwa upande wake Silver alikana kuombwa msamaha na Klopp akisema yeye hakumuona mtu yeyote kumfuata na kumuomba msamaha baada ya mchezo ule kwa tukio lolote lile.

“Kusema ukweli sijamuona Klopp wala mtu mwingine yeyote kuja kuniomba msamaha hata hivyo mimi sijali kwa yaliyotokea,” alisema.

Alisema kwamba mchezo ulikuwa mzuri wenye ushindani na vijana wake walikaribia kuondoka na pointi moja lakini bahati haikuwa upande wao kwani walipoteza mchezo dakika ya mwisho kabisa ya mchezo.

Matokeo hayo yameifanya Liverpool iendelee kubakia katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 36 mbili chini ya vinara Manchester City zote zikiwa zimecheza mechi 14.

Timu hizo mbili zinazochuana kileleni ndizo pekee ambazo hazijapoteza mchezo hadi sasa tangu kuanza kwa Ligi hiyo Agosti mwaka huu.