Nicolas Pepe popote anakwenda kuliamsha

Muktasari:

Pepe amefunga mabao 23 katika mechi 45 za michuano yote aliyocheza msimu uliopita, huku akiwa sehemu muhimu ya kikosi cha Lille kilichomaliza nafasi ya pili kwenye Ligue 1.

PARIS, UFARANSA.WAKALA wa staa Nicolas Pepe amesema mteja wake huyo yupo tayari kutua popote pale iwe Manchester United au Arsenal ili tu akakipige kwenye Ligi Kuu England.
Ripoti zinadai kwamba miamba hiyo ya Ligi Kuu England inapigana vikumbo kwenye kusaka huduma ya mshambuliaji huyo wa Lille, huku mabingwa wa Ufaransa, Paris Saint-Germain nao wakifukuzia saini yake.
Lakini, wakala wa mchezaji huyo alisema Pepe mwenyewe kinachomvutia kwa sasa ni kwenda kwenye Ligi Kuu England.
Wakala Samir Khiat, alisema: "Nicolas milango yake iko wazi. Jambo kubwa kwake ni kusaini kwenye timu mwafaka. Wanaweza kuwa PSG pia.
"Pande zote zinahitaji kufikia makubaliano. Kumekuwa na majadiliano na mijadala. Timu ni nyingi zinazomtaka.
"Yeye anachotaka ni kwenda kujiunga na timu nzuri, ambayo atachezanna kuendelea kukuza kiwango chake cha soka."
Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer ameripotiwa kumtaka staa huyo wa Ivory Coast ili kwenda kusaidiana na washambuliaji Marcus Rashford na Anthony Martial -kama Romelu Lukaku, ataondoka kutokana na matakwa yake ya kwenda Inter Milan.
Arsenal, wao kwa upande wao wanahitaji kutengeneza safu ya washambuliaji watatu baada ya sasa kuwa na Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette. Lakini, shida ni PSG ambao bila ya shaka watakuwa na pesa za kumsajili wanayemtaka kama watamuuza Neymar kwa ada ya Pauni 200 milioni.
Pepe amefunga mabao 23 katika mechi 45 za michuano yote aliyocheza msimu uliopita, huku akiwa sehemu muhimu ya kikosi cha Lille kilichomaliza nafasi ya pili kwenye Ligue 1.