Ni moto kwa moto Ligi Kuu England

LONDON, ENGLAND. WAACHE wauane. Frank Lampard na Jurgen Klopp wanakabiliwa na mtihani mzito kesho Jumapili wakati vikosi vyao Chelsea na Liverpool vitakapoonyeshana ubabe kwenye mchezo wa Ligi Kuu England utakaopigwa uwanjani Stamford Bridge.

Kipute hicho kinatarajia kuwa na upinzani mkali kwelikweli, ambapo safu ya mabeki ya Liverpool inayoongozwa na Virgil van Dijk itakuwa na shughuli pevu kuwadhibiti washambuliaji wa Chelsea, wakiongozwa na Timo Werner, Kai Havertz, Hakim Ziyech na Mason Mount.

Kwa upande wa mabeki wa The Blues watakaowaongozwa na Thiago Silva watakuwa na kasheshe la kuwadhibiti Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino. Mechi hiyo inabeba taswira ya mapema katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England. Kwa msimu uliopita, timu hizo ziliachana kwa pengo kubwa la pointi, hivyo upinzani ni mkali.

Wakati kipute hicho kikisubiriwa kwa hamu, mchakamchaka wa ligi hiyo utaendelea leo ambapo Manchester United ikitarajiwa kuwa na huduma ya staa wao mpya, Donny van de Beek kwa mara ya kwanza kabisa kwenye ligi, watacheza mechi yao ya kwanza kwa kuwakaribisha Crystal Palace uwanjani Old Trafford, wakati Arsenal ilioangusha kipigo kwenye mchezo wao wa kwanza itakuwa nyumbani Emirates kukipiga na West Ham United wababe wenzao wa London.

Everton ya staa James Rodriguez baada ya kuichapa Tottenham Hotspur kwenye mchezo wa kwanza itakuwa nyumbani Goodison Park kukipiga na West Brom, huku watoto wa Marcelo Bielsa, Leeds United baada ya kuwapelekapeleka mchakamchaka Liverpool kwenye mchezo wa kwanza watakuwa nyumbani kucheza na Fulham. Mechi nyingine za ligi hiyo zitakazopigwa kesho, Jose Mourinho na chama lake la Spurs baada ya kuchapwa kwenye mchezo uliopita wakiwa nyumbani itakuwa ugenini kwa Southampton huku Newcastle United ikiwa nyumbani kuwakaribisha Brighton na Leicester City ya Brendan Rodgers na Jamie Vardy itajimwaga kwenye uwanja wao wa nyumbani wa King Power kucheza na wagumu Burnley.

Keshokutwa Jumatatu kutakuwa na mechi mbili, ambapo huko Villa Park wenyeji Aston Villa itakuwa na kasheshe la kuwakabili Sheffield United, wakati Wolves itakuwa nyumbani kumkaribisha Pep Guardiola na jeshi lake la Manchester City litakalokuwa na huduma matata kabisa ya wakali wake akiwamo Kevin de Bruyne na Raheem Sterling. Hii ni wiki ya pili kwenye mikikimikiki hiyo, lakini kwa vigogo Man City na Man United zitacheza mechi zao za kwanza baada ya kuahirishiwa michezo ya kwanza baada ya kuchelewa kutoka kwenye michuano ya Ulaya, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Europa League.