Nani alipoyakanyaga!

Manchester ENGLAND. VIJIMAMBO vya Luis Carlos Almeida da Cunha. Unamkumbuka? Yule winga wa Kireno aliyetamba sana Manchester United. Walimwita Nani.

Mwenyewe anasema kama kuna kitu anajutia, basi ni pale alipochukua uamuzi wa kuhama timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford, mwaka 2015.

Nani anakwambia mwaka 2010 aliyakanyaga. Katika mchezo mmoja wa ligi, Man United ikiwa mbele kwa 2-1 dhidi ya Fulham, wababe hao wa Old Trafford wakapata penalti ya kufunga chuma cha tatu. Nani, akajifanya ubabe, akamnyang’anya Ryan Giggs mpira na kupiga yeye penalti hiyo. Mungu si Athumani, Nani kakosa penalti na baadaye, Fulham wakaja kusawazisha, mechi ikamalizika kwa sare ya 2-2. Unaambiwa, Sir Alex Ferguson alifyumu balaa.

Mbaya zaidi, Nani na Ferguson walikuwa wakiishi majirani.

Hivyo, baada ya mechi, Nani alikuwa na jukumu la kumrudisha Ferguson hadi kwake.

Basi unaambiwa, Nani mwenyewe anasema alimpa lifti Ferguson hadi kwake baada ya mechi hiyo, lakini kocha huyo hakumsemesha Nani kitu chochote kile, hata alipofika alishuka na kuondoka zake.

Kwanza Ferguson alimbwatukia Nani kwenye vyumba vya kubadilishia na kisha walipokuwa wote kwenye gari kutoka Stockport hadi Wilmslow, hakumsemesha kitu chochote, amemnunia. Kisa ni ile penalti aliyokosa, ambayo ilipaswa kupigwa na Giggs.

“Ferguson alikuwa jirani yangu na tulikuwa tukisafiri sana na treni kwenda London,” alisema Nani.

“Mkewe au familia yake walikuwa wakimwaacha kwenye treni, hivyo suala la kurudi nyumbani kwake alikuwa hana dereva, hivyo alikuwa akisubiri lifti za watu anakaa nao jirani wampandishe. Hivyo, nikamwambia, ‘oke bosi, usajili nitakuwa nakupeleka nyumbani’. Lakini, siku niliyolazimika kumpeleka nyumbani ilikuwa majanga!

“Siku hiyo ilikuwa baada ya mechi dhidi ya Fulham. Mimi nilianzia benchi na baada ya kuingia nilikuwa najiamini sana. Tukapata penalti na Giggs ndiye aliyepaswa kupiga. Nikaonyesha kujiamini na Giggs hakusema kitu. Nikapiga penalti, nikakosa!

“Tulivyoingia vyumbani, Ferguson alinichana kinoma. Alisema, ‘Nani, hivi wewe unajikuta nani kwa mfano? Nani kakupa ruhusa ya kupiga penalti?. Kisha akamgeukia Ryan Giggs, akasema, ‘Ryan, kwa nini umemruhusu apige penalti?’.

Ryan akajibu, ‘amechukua mpira na mimi nikamwacha apige’. Mungu wangu, siku hiyo ilikuwa balaa.

“Wakati nampeleka nyumbani siku hiyo, hakuzungumza na mimi kitu chochote kwenye gani. Yani nilikuwa kwenye wakati mgumu kwelikweli.”

Kuhusu Man United, Nani anafichua aligomea timu nyingi sana ikiwamo Arsenal wakati alipochagua uamuzi wa kutua Old Trafford mwaka 2007.

Akiwa na Man United, Nani ameshinda mataji manne ya Ligi Kuu England na taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika misimu yake saba aliyodumu huko Old Trafford.

Timu nyingine ambazo Nani amezigomea ni Chelsea, Real Madrid huku akidai Bayern Munich, Juventus na Inter Milan zilikuwa kwenye orodha pia ya kunasa saini yake. Nani kwa sasa anachezea Orlando City ya Marekani.