Mwakinyo: Tulieni hachomoki

Muktasari:

Mabondia Watanzania, Hassan Mwakinyo na Iddi Mkwera atazichapa leo pambano la utangulizi dhidi ya Nicholas Mwangi.

BONDIA Hassan Mwakinyo ana dakika 24 za kuweka historia nyingine kwenye ndondi atakapopanda ulingoni kuzichapa na Muargentina, Sergio Eduardo Gonzalez.

Pambano hilo lililobeba hisia za mashabiki wa ndondi ndani na nje ya nchi litapigwa usiku wa leo Jumamosi, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) jijini Nairobi.

Jana Ijumaa, Mwakinyo na Gonzalez walipima uzito na afya tayari kupanda ulingoni, pambano la dakika 24 ambalo ni la kwanza kwa Mwakinyo kucheza nje ya Tanzania tangu alipomchapa Sam Eggington wa Uingereza kwa pointi nchini Uingereza mwaka jana.

Akimzungumzia mpinzani wake, Mwakinyo alisema ni bondia mzuri, mwenye uzoefu wa kutosha, lakini kwa namna alivyojiandaa chini ya SportPesa, hawezi kupigwa.

“Nataka niweke rekodi zaidi ya ile niliyoiweka England,” alisema Mwakinyo ambaye alimchapa kwa TKO raundi ya pili Egginton na kupata umaarufu sanjari na kupanda katika viwango vya ubora wa dunia.

Mwakinyo alisema licha ya uzoefu wa mpinzani wake, lakini, Gonzalez atake asitake, lazima akae mapema watakapozichapa pambano la raundi nane la uzani wa super welter kuwasindikiza, bingwa wa dunia wa WBC, Fatuma Zarika atakayekuwa akitetea taji lake dhidi ya Catherine Phiri katika uzani wa bantam.

“Nahitaji kuendeleza rekodi yangu ya ushindi wa TKO mfululizo, Sportpesa iliponipeleka kambini Uingereza ilikuwa na maana kubwa, hivyo Muargentina ajiandae, huenda ikawa rekodi zaidi ya ile niliyoiweka pambano na Eggington,” alisema Mwakinyo

Mbali na Mwakinyo, Mtanzania mwingine, Iddi Mkwera atazichapa leo pambano la utangulizi dhidi ya Nicholas Mwangi.