Mwakilema: TFF hawaijui Yanga, watuachie timu yetu

Muktasari:

Katibu Mkuu wa tawi la wanachama wa Yanga Ubungo Terminal, Stephen Mwakilema amesema kuwa kitendo cha Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Soka Tanzania (TFF) kusimamia uchaguzi wao bila ya kuwa na rejea ni kuvunja katiba ya klabu yao.

KATIBU Mkuu wa tawi la wanachama wa Yanga Ubungo Terminal, Stephen Mwakilema amesema kuwa kitendo cha Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Soka Tanzania (TFF) kusimamia uchaguzi wao bila ya kuwa na rejea ni kuvunja katiba ya klabu yao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwakilema alisema kuwa kamati ya TFF wanatambua vipi kama Wanayanga wanaochukua fomu za kuwania uongozi katika klabu hiyo ni hai bila kuwa na rejea ambayo inawafahamisha hilo.

Alisema kigezo chao cha kuchukua fomu zikiwa zimeambatana na kadi ya uanachama hakisaidii kuwa na uhakika, kwa sababu kila mwanachama ana kadi lakini kuwa wanachama hai na wafu kutokana na kadi hizo kulipiwa na wengine kushindwa kufanya hivyo.

“Uchaguzi huo wanaotaka kuusimamia wao watachaguana wao wenyewe sisi kama wanachama hai wa Yanga tunaendelea na maamuzi ya Mkutano Mkuu ambayo yanamtambua Mwenyekiti wetu, Yusuf Manji na tumebakiwa na jukumu moja tu la kuziba nafasi za Makamu Mwenyekiti na wWajumbe wanne,”

“TFF ina mambo mengi ya kuyashughulikia mfano ni hili suala la Wambura linawapa shida, timu ya Taifa inashindwa kufanya vizuri, hayo yanawashinda halafu wanaizungumzia Yanga, watuachie timu yetu na hakuna mtu aliye juu ya katiba yetu,” alisema katibu huyo.