Mtoko mpya wa Solskjaer ni huu

Muktasari:

Hata hivyo, Kocha Ole Gunnar Solskjaer wala hayupo kwenye hatari ya kupoteza kibarua chake huko Old Trafford.

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER United imetumia Pauni 150 milioni kusajili kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi, lakini kiwango bado kipo chini sana.


Kwa sasa kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, wapo juu kwa pointi mbili tu kutoka kwenye shimo la kushuka daraja baada ya mechi nane na hilo linaweka wazi kwamba mambo yamekuwa hayaendi vyema.


Hata hivyo, Kocha Ole Gunnar Solskjaer wala hayupo kwenye hatari ya kupoteza kibarua chake huko Old Trafford.


Ripoti zinadai bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo inafahamu kwamba Kocha Solskjaer amekuwa na kazi ngumu sana, hivyo wanamtaka Makamu Mwenyekiti, Ed Woodward kumpatia muda na mambo mengine anayotaka ili kubadili hali ya mambo.


Kwa mujibu wa ripoti hizo hizo zinadai kwamba, Woodward amepitisha usajili wa wachezaji wanne, ambao watanaswa kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kuirudisha Man United kwenye makali yake. Na kama dili hizo zitakwenda kama zilivyopangwa, basi hivi ndivyo Man United itakavyokuwa msimu ujao.


Golini, atakuwapo kipa namba moja, David de Gea wakati beki wa kulia ni Aaron Wan-Bissaka na kushuto atakuwa Ben Chilwell, atakayenaswa kwenye dirisha hilo la majira ya kiangazi kama itakavyokuwa kwa Kalidou Koulibaly, ambaye atakuja kuungana na Harry Maguire kutengeneza kombinesheni matata kwenye beki ya kati.

Viungo wa kati watakuwa Scott McTominay na Paul Pogba na kwenye fowadi kutakuwa na nyota wapya wawili, James Maddisonn na Moussa Dembele watakaoungana na Anthony Martial na Daniel James.

Hapo, Marcus Rashford atakuwa anatokea benchi, sawa na wakali wengine akiwamo Mario Mandzukic, anayedaiwa kwamba huenda akatua Old Trafford kwenye dirisha la Januari.