Mtanzania kilingeni kusaka medali Argentina

Muktasari:

Timu ya Tanzania inatupa karata ya kwanza leo Jumatatu ambapo muogeleaji Sonia Tumiotto atashindana kwenye mtindo wa freestyle mita 100 leo Jumatatu. Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michezo hiyo ya Olimpiki kwa timu za vijana inayofanyika Argentina ni Denis Mhini na wanariadha Regina Mpigachai na Francis Damiano.

Dar es Salaam. Timu ya Tanzania inayoshiriki michezo ya vijana Olimpiki imewasili salama Argentina na kushiriki hafla ya ufunguzi wa michezo hiyo.

Hafla ya ufunguzi iliongozwa na Rais wa Argentina, Mauricio Macri kwenye Uwanja wa Obelisco de Buenos Aires.

Muogeleaji Sonia Tumiotto atafungua pazia kwa Tanzania atakapotupa kete ya kwanza kwenye mtindo wa freestyle mita 100 leo Jumatatu.

Akizungumza kwa simu jana Kocha wa timu hiyo, Michael Livingstone alisema Sonia yuko katika kiwango bora tangu walipowasili Argentina Alhamisi iliyopita.

Livingstone alisema ana matumaini Sonia atafanya vyema katika kwa kuwa ameonyesha kiwango bora katika maandalizi aliyofanya kabla ya kwenda Argentina.

"Tulifanya mazoezi mepesi ya siku mbili Ijumaa na leo (jana) Jumapili tumetumia vifaa vya kisasa vilivyopo huku, ambavyo vimetuongezea morali ya ushindani, vijana wangu wote wako fiti na bila shaka Sonia ataanza vizuri kuifungulia njia Tanzania kesho (leo)," alisema kocha huyo.

Muogeleaji mwingine, Denis Mhini atapambana kesho katika mtindo huo kwa umbali wa mita 100 kabla ya waogeleaji hao kuchuana kwa mtindo wa backstroke kati ya Jumatano na Alhamisi.

Mbali na waogeleaji, wanariadha, Regina Mpigachai anayechuana katika mbio za kati (mita 800) na Francis Damiano mbio ndefu za uwanja (mita 3,000) watasaka medali kati ya Ijumaa na Jumamosi.

Wakati Damiano atachuana kwenye fainali moja kwa moja na Regina ataanzia katika mchujo wa michezo hiyo.

Kocha wa riadha, Mwinga Mwanjala alisema ana imani wakimbiaji wake watafanya vizuri kutokana na maandalizi waliyofanya na muda ambao watatumia kumaliza mbio.

"Damiano yuko katika kiwango bora, ameweza kupunguza muda wake ule aliokimbia kwenye mbio za Jumuiya ya Madola ambako alishinda medali ya shaba, hivyo sina wasiwasi nae, japo Regina naye anayo nafasi ya kufanya vizuri na kuboresha muda wake," alisema Mwinga.