Msimbazi yainasa Nkana FC kiulaini

Muktasari:

  • Kocha Aussems amesema tayari ameshayanasa mafaili yote ya wapinzani wake Nkana Rangers na kilichokuwa mbele yake ni kwenda kuyafanyia kazi.

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Simba na Mtibwa Sugar jana Alhamisi zilipishana kwa dakika tano tu kutua kwa ndege nchi wakitokea nje ya nchi walipoenda kucheza mechi zao za marudiano ya michuano hiyo ya CAF.

Simba ilitua jana ikitokea eSwatini ilipoing’oa Mbabane Swallows saa 8:50 mchana dakika kama 10 tangu Mtibwa ilipowatangulia kwa kutua ikitokea Shelisheli ilipoenda kuitupa nje Northen Dynamo katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems akafichua siri nzito ya wapinzani wao katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Nkana FC ya Zambia akidai hawajui, lakini tayari mafaili yao yote yapo mezani mwake.

Kocha Aussems alisema mara baada ya kusikia Nkana imeshinda ugenini mabao 2-1 dhidi ya UD Songo ya Msumbiji katika mechi yao ya kwanza na wakwatakutana na moja ya timu hizo, alianza kuifuatilia kwa undani Nkana ili kuwasoma mapema.

Simba, itavaana na Nkana kati yaDesemba 14-16 nchini Zambia kabla yua kurudiana nao wiki moja baadaye jijini na Dar es Salaam na mshindi atatinga moja kwa moja katika makundi na mshindwa ataangukia katika playoff ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha Aussems alisema tayari ameshayanasa mafaili yote ya wapinzani wake Nkana Rangers na kilichokuwa mbele yake ni kwenda kuyafanyia kazi.

“Katika maisha yangu ya ukocha sijawahi kucheza na Nkana, ila nafahamu sasa hivi ndio mpinzani wangu natakiwa kujiandaa kikamilifu ili nitakapokutana nao niweze kufanya vizuri,” alisema Aussems.

“Nimeshaanza kuwaandaa vijana wangu kwa ajili ya mechi hiyo na maandalizi yalianza kule kule eSwatini ambapo mara baada ya kumaliza mechi tulifanya mazoezi katika uwanja ule siku moja mbele.

“Ratiba imekaa vizuri kwetu kwa kuanzia mechi ya kwanza kuanza kucheza ugenini na kumalizia hapa nyumbani, pia kutokucheza mechi za ligi itatupa nafasi ya kujianda vyema.”

Naye Nahodha Msaidizi wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alisema kazi ambayo walikuwa wanataka kuifanya katika mechi ya kwanza dhidi ya Mbabane Swallows wameifanikisha na akili yao ni katika mechi inayofuata. Kwa upande wa viongozi wa Simba, Mwenyekiti Swedi Mkwabi na Mjumbe wa Bodi, Salim Abdallah ‘Try Again, walisema kama uongozi umefurahishwa na kazi nzuri ambayo wameifaanya wachezaji wao katika mechi na Mbabane kwa kupata ushindi wa maana katika mechi zote mbeli na kusonga mbele.

Aidha Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema wmefurahi kuvuka raundi ya awali na sasa wanaendelea na nia yao ya kutaka wafike mbali katika michuano hiyo kwa kujiandaa vizuri kabla ya kuifuata KCCA ya Uganda wiki ijayo.

“Tunatambua tumepangwa kukutana na timu ngumu, hivyo hata maandalizi yetu yatakuwa ya aina yake tukianzia Dar kabla ya kwenda kuweka kambi ya muda mfupi Bukoba, kabla ya kuwafuata wapinzani wetu,” alisema Katwila.