Mpoto kuwatembeza watu pekupeku

MWANAMUZIKI Mrisho Mpoto ‘Mjomba’ ametambulisha mpango utakaotambulika kama ‘Mapinduzi ya Kimkakati’ atakaouzindua hivi karibuni ili kila Mtanzania afahamu dhumuni la jambo hilo.

Mpoto anasema Mapinduzi ya Kimkakati ni ajenda kubwa ambayo itahusu watu wengi wanaomuishi Rais wa Kwanza Tanzania Mwl. Julius Kambarage Nyerere lakini hawafanyi yale aliyokuwa anafanya kwahiyo anataka kuona miaka 20, kabla na baada ya kufa kwake tupo wapi. Tunakwenda kutengeneza mjadala wa kitaifa kuhusu hilo.

Mpoto anasema Nyerere alizikwa chini ya ardhi kwahiyo siku ya tukio anaomba kila ambaye atakayefika kuungana nao asivae viatu kwa maana ya kuwa ‘pekupeku’ kwani huo ndiyo utamaduni wa Mtanzania.

“Ningeomba bila kujali wadhifa au nafasi yako katika jamii, siku ya tukio tufike sote tukiwa pekupeku na Jumatatu ndiyo nimetambulisha jambo langu hapa Mwananchi Communications Limited na bila kuficha nimefurahi sana Mkurugenzi Mtendaji wa hapa, Francis Nanai amenielewa na kuungana nami katika harakati yangu hii,” anasema.

“Siku hiyo ya uzinduzi wa tukio la Mapinduzi ya Kimkakati tutakwenda kujadili mambo ya kabla na baada ya miaka 20 ya Mwalimu Nyerere, na mada kubwa ni kumfahamu mwasisi wa taifa hili alikuwa na mchango upi na kila tasnia kama waandishi habari, wasanii, wanamuziki na wachambuzi, kila upande useme yao ya msingi.

“Kubwa ambalo litatukutanisha katika tukio hilo ni kazi ya fasihi ambayo tunaiandika kila siku na lengo likiwa ni kuelimisha jamii katika mambo yote ya msingi kulingana na mchango alioutoa Nyerere na alivyokuwa anaishi lakini pia, kutakuwa na uzinduzi wa wimbo wetu ambao utahusu ajenda nzima ya Mapinduzi ya Kimkakati na kutakuwa na zawadi nyingi ambazo zitatolewa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Nanai,” anasema Mpoto ambaye Jumatatu alitembelea ofisi za Mwananchi zilizopo Tabata Relini hapa Dar es Salaam.

“Baada ya uzinduzi wa mpango wa kimkakati tunataka kuona kila Mtanzania anapata walau muda wa kuishi na kuyafanya yale ambayo alikuwa akiyafanya Nyerere kabla na baada ya miaka 20. Nafahamu si rahisi jambo hili kueleweka kwa haraka lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda nina imani wananchi watafahamu juu ya hilo,” anasema msanii huyo ambaye daima hutembea pekupeku.

MASHARTI YA MGANGA?

Kufanikiwa kimuziki na kimaisha, kunamsababishia Mpoto maswali mengi anapoonekana akiteremka peku katika gari yake kali anayomiliki.

Wengine wanaamini kwamba Mpoto ametembea peku kutimiza masharti ya mganga ili afanikiwe katika kazi zake, jambo ambalo halina nafasi kwa muimbaji huyo mashuhuri wa ghani.

Mpoto anasisitiza staili ya kutembea peku licha ya faida kadhaa anazozitaja kiafya, pia ni utambulisho wake kama ilivyo kwa rasta zake anazofuga kichwani.

“Binafsi nafikiria kugusana mwili wangu na ardhi kuna faida nyingi, mbali na wazee wetu kuishi miaka mingi, maradhi huwa mbali nao na walikuwa na uwezo wa kuzaa watoto 12 hadi 15,” anasema.

“Kizazi hiki cha sasa tunashindwa kufanya hivyo na tunaandamwa na matatizo mengi ya kiafya kutokana na mifumo yetu ya sasa, imekaa kiteknolojia zaidi.

“Ukitembea bila viatu tena unyayo ukigusana na ardhi kuna afya na maarifa mengi yanaongezeka katika mwili wa binadamu jambo ambalo hivi sasa halifanyiki, ndiyo maana nimepanga kulihamasisha walau kwa muda mchache kwa siku tuweze kutembea peku,” anasema.

“Kuhusu kufuga rasta nalo familia yangu wala haina shida nalo kama ilivyo kwa kutembea bila viatu. Ni miongoni wa utambulisho wangu wa haraka,” anasema Mpoto.

Mpoto nasema katika imani yake rasta zake wala hazina shida kwani hizo ni nywele zake binafsi wala hajaongeza na kitu kingine labda ingekuwa tofauti na hivyo ndiyo kungekuwa na shida katika imani yake.

“Sina gharama za ziada kwa nywele zangu. Ninachojigharamia mimi kwa siku ndiyo gharama ya mahitaji ya nywele zangu kwani ni sehemu ya mwili wangu,” anasema.

ANATUNGIWA NYIMBO

Mpoto amekuwa akitungiwa nyimbo zake kadhaa zinazotamba na anasema haoni tatizo kuhusu hilo.

“Sioni tatizo kushauriana na mtu ambaye amepiga hatua katika elimu au jambo fulani kwa sababu inaongeza ufanisi wa kazi yangu na dhamira yangu ya kufikisha ujumbe ulioshiba.

“Sijali wimbo nimeandika mimi ama siyo mimi. Nia yangu ni ujumbe ninaotaka ufike na ulete mjadala mkubwa katika jamii, lengo likiwa ni kuelimisha kulingana na ujumbe uliokuwapo, lakini kujali kama nimetungiwa au nimetunga mwenyewe hilo kwangu wala halinisumbui,” anasema.

“Hata kama imetokea nami nimetunga wimbo kuna msaniii mwingine akautumia na ukafanya vizuri kwa ujumbe kufika kwa jamii hilo ndiyo linatakiwa na si kuanza kumpa sifa yule ambaye ametunga wimbo wenyewe, kinachotakiwa ni yale matokeo. Ndiyo maana siku zote kazi zangu huwa haziuzwi na kama ikitokea nauza ni kutakana na changamoto za maisha,” anasema.

YUKOJE NA SANGA

Miongoni mwa nyimbo ambazo Mpoto ameimba na zimetamba ni ‘Salamu Zangu Mjomba’ ambao ulitungwa na msanii, Irene Sanga.

Ni wimbo huo ndiyo uliomtoa Mpoto kisanii nchini na kujikuta yeye mwenyewe akipachikwa jina la utani la ‘Mjomba’.

Akimzungumzia mtunzi wa wimbo huo uliompa maisha, Mpoto alisema alimpokea mwanamama huyo wakiwa Bagamoyo katika chuo cha sanaa kabla ya kushirikiana katika kazi walipokuwa pamoja katika Kundi la Parapanda Arts chini ya Mgunga Mwamnyenyelwa.

“Baada ya hapo nilipata safari ya kwenda Uingereza na niliporudi nchini ndiyo tukafanya kazi moja ambayo baadaye ndiyo yakaja kutokea ambayo yametokea hadi leo, lakini zaidi ya hapo hakuna kingine kati yangu mimi na Irene, naomba jamii ielewe hivyo,” anasema Mpoto.

FEDHA, ELIMU

Mpoto ambaye amepata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Boma, Ilala, Dar es Salaam anasema anajua watu wanapenda kufahamu mambo mengi binafsi yanayowahusu watu maarufu ikiwamo vipato vyao, mke mzuri au elimu kubwa, lakini yeye hapendi hayo yafahamike bali anataka usikike ujumbe wake tu.