Mourinho, Chelsea watoleana siri zao

Muktasari:

Kitu kibaya zaidi, Messi alikuwa ametoka katika majeraha na nyaraka zinadai Mourinho aligundua hilo na alitaka staa huyo achezewe rafu mara kwa mara.

HALI si shwari kati ya kocha wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England. Kuna siri zinafichuka baina yao na kila mmoja anamsukumizia mwenzake mzigo.

Mourinho amechukia vikali baada ya nyaraka kuvunja zikidaiwa ni zake zikionyesha jinsi ambavyo Chelsea ilikuwa inajiandaa kuikabili Barcelona katika pambano la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya mwaka 2006.

Wakati huo Barcelona ilikuwa inafundishwa na kocha wao wa zamani Mdachi, Frank Rijkaard na Mourinho anaonekana kuandaa mbinu za kukikabili kikosi cha kocha huyo huku akiamuru kinda, Lionel Messi aliyekuwa na umri wa miaka 18 wakati huo achezewe rafu nje ya boksi.

Kitu kibaya zaidi, Messi alikuwa ametoka katika majeraha na nyaraka zinadai Mourinho aligundua hilo na alitaka staa huyo achezewe rafu mara kwa mara.

“Kama inabidi kumchezea faulo basi ni muhimu kufanya hivyo nje ya boksi mapema kwa sababu ndio amerudi kutoka katika majeraha,” ilisema nyaraka hiyo ambayo inadaiwa kuandikwa na Mourinho.

Nyaraka hiyo pia iliandika kuwa ‘Barcelona watajiangusha sana kudai faulo na penalti’ huku ikidai Mlinzi wa Mexico, Rafael Marquez ‘Anapenda kudanganya kuguswa sana’ na ilidai Ronaldinho ‘Alikuwa muongo kwa waamuzi’.

Mlinzi wa kushoto wa Barcelona, Sylvinho ambaye ni staa wa zamani wa Arsenal alitajwa kuwa kama sehemu dhaifu katika safu ya ulinzi ya Barcelona kwa sababu ‘Hakujua namna ya kujilinda’.

Nyaraka hiyo pia ilidai beki mkongwe, Carles Puyol alikuwa ‘anapenda kubwatukia waamuzi’ huku ikidaiwa kwamba staa huyo alikuwa kiongozi dhaifu uwanjani na hakuwa anajua kukaa vyema katika eneo la ulinzi.

Kwa jumla Chelsea ilipoteza mechi hizo mbili kwa idadi ya mabao 3-2 huku mlinzi wao wa kushoto, Asier Del Horno akitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya Messi katika kibendera cha kona.

Sasa Mourinho amezijia juu nyaraka hizo zilizovuja kutoka kwa watu wa Chelsea akidai kwamba hazikuandikwa na yeye.

“Samahani kwa kuwaudhi wale wote wanaodhani kwamba niliandika nyaraka hizo. Sikufanya hivyo.

“Hizo ripoti sio zangu. Sikuziandika. Nyaraka yangu ya mwisho niliyoandika ninayo nyumbani. Nilikuwa Barcelona katika msimu wa 1999/2000,” alisema Mourinho.

“Nilikuwa msaidizi na nilichangia kuandika na wenzangu masuala ya uchambuzi na mbinu kwa ajili ya kumuandalia kocha. Tangu nilipowasili Benfica na mpaka sasa uchambuzi wangu kamwe haukai kama ripoti rasmi, lakini kuna mawazo muhimu ambayo yalinisaidia katika kuandaa mazoezi na mipango ya mechi.

Ripoti rasmi zilikuwa zinaletwa na wachambuzi, wasaidizi, mafundi wa kompyuta lakini sio mimi,” aliongeza Mourinho.

Watu wa karibu wa Mourinho ambaye ni kocha wa zamani wa Porto, Inter, Real Madrid na Manchester United wanadai kocha huyo amechukia kuhusu kusingiziwa aliandaa ripoti hiyo lakini bado haijajulikana kama atachukua hatua za kisheria.

Uhusiano kati ya Mourinho na watu wa Chelsea unaonekana kudorora kila kukicha huku pia mashabiki wa timu hiyo wakimzomea mara kwa mara pindi anapokwenda katika uwanja huo na timu nyingi.

Mara ya mwisho alipokwenda Stamford Bridge akiwa na Manchester United kocha huyo alizomewa huku akitoa ishara ya vidole vitatu kwa mashabiki wa timu hiyo akimanaanisha yeye ndiye kocha aliyewapa mataji matatu ya Ligi Kuu klabuni hapo.