Yanga na Morrison kibao kimegeuka

Friday July 3 2020

 

By WAANDISHI WETU

MAMBO bado ni moto. Lile sakata la winga Bernard Morrison na Yanga juu ya ishu ya mkataba mpya wa miaka miwili, bado utata huku ikielezwa tayari kuna vigogo wa soka nchini wametaka kutia mkono na kupata upinzani kutoka kwa watu wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.

Baada ya kuvuja juu ya suala la vigogo hao wa soka, Shirikisho la Soka (TFF) jana jioni likaamua kutoa taarifa yake likiruka kimanga na kudai kamati hiyo na nyingine za shirikisho hilo zinafanya kazi zao bila kuingiliwa taarifa hiyo ya TFF ilisainiwa na Ofisa Habari wao, Clifford Ndimbo.

Hata hivyo, mapema mchana Mwanaspoti lilipenyezewa taarifa kwamba Kamati hiyo ya Sheria chini na Mwenyekiti wake, Elias Mwanjala tayari ilishatoa maamuzi kwa baadhi ya kesi zilizokuwa mbele yake ikiwamo lile sakata la Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela na kiungo wa Simba, Clatous Chama pamoja na ile ya Morrison na Yanga na kilichobaki ilikuwa ni kutangaza.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kikao hicho ni kwamba mmoja wa vigogo wa soka nchini, ni kama alitaka kuinunua kesi hiyo kwa Morrison hasa baada ya kubainika kwamba kuna dalili zote kwamba winga huyo Mghana alisaini mkataba mpya na Yanga, ila anajitoa fahamu tu.

Chanzo hicho kinasema, kwa ushahidi na maswali aliyoulizwa Morrison na kamati hiyo na ule uliotolewa na mabosi wa Yanga, ni wazi winga huyo ni kama anazingua na ikaelezwa kama kweli anadhani kuna udanganyifu aliofanyiwa juu ya saini yake inafaa aende kwenye vyombo vya kisheria.

Hata hivyo, chanzo hicho kinasema wakati kamati ikijiandaa kutaka kutoa taarifa rasmi jioni baada ya kikao cha siku ya pili kumalizika, lakini ikakanwa kwa madai ya kuwepo kwa maelekezo mapya kutoka kwa vigogo wa TFF ambao inadaiwa wametaka suala hilo walisimamie wao.

Advertisement

Hali hiyo inaelezwa imefanya wajumbe wa kamati kupaniki na kusimamia msimamo wao juu ya walichokiona kwenye kesi hiyo na hata ile ya Chama na Mwakalebela walipotaka walalamikaji wakajipange upya ili kuweza kuleta shtaka upya.

Inadaiwa hilo ndilo lililosababisha wakashindwa kutolea taarifa juu ya kesi hizo kama walivyokuwa wamepanga awali na Mwenyekiti wao, Mwanjala alipotafutwa jioni aliomba apewe muda kabla ya kutoa taarifa, lakini mpaka tunaenda mitamboni hakufanya hivyo, huku simu yake ikipigwa na kuita bila kupokewa.

Morrison na Yanga wamefikishana TFF kupingana juu ya mkataba mpya wa miaka miwili, mchezaji akidai hajasaini, huku viongozi wakidai aliusaini kupitia mdhamini wao GSM mbele ya wanasheria ambao walikubaliana kila kitu na kilichokuwa kinasubiriwa ni fedha.

Hata hivyo, inaelezwa fedha walizokubaliana zilishaingizwa kwenye akaunti, huku ikidaiwa Morrison amezikataa na kudai hajui waliomwekea na kutaka zirudishwe, lakini ikielezwa msimamo wa Mghana huyo umetokana na mzigo aliowekewa na wapinzani wa Yanga wanaodaiwa wanataka kumsajili.

Juzi, Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Masingiza alikanusha taarifa kwamba klabu yao imezungumza na kumshawishi Morrison kujiunga nao kwa madai kwamba wanaelewa ana mkataba Jangwani.

Advertisement