Mmesikia? Mo Salah, Mane wataondoka tu

LIVERPOOL, ENGLAND. HABARI ndo hiyo. John Barnes, amesema Liverpool hawatakuwa na ujanja wa kuwazuia mastaa wake, Mohamed Salah na Sadio Mane wasiondoke kwa sababu mkwanja ambao utawekwa mezani kwa ajili ya wachezaji hao itakuwa ngumu kuugomea.

Mkali huyo wa zamani wa Liverpool, Barnes alisema hilo limekuwa kawaida kwa timu hiyo kushawishika na kuuza nyota wake pindi wanapowekewa mezani ofa tamu.

Mastaa Luis Suarez na Philippe Coutinho wote waliondoka kwenye timu hiyo kwenda kujiunga na Barcelona wakiwa kwenye viwango vikubwa kwa sababu tu, pesa iliyowekwa mezani ilikuwa ngumu kuigomea.

Kikosi hicho cha Jurgen Klopp kwa sasa kina mastaa kibao wa kiwango cha dunia, wakiwamo Mo Salah na Mane, ambao wamekuwa kivutio kikubwa kwa klabu vigogo duniani, hasa miamba ya Hispania, Barcelona na Real Madrid.

Na Barnes anawapa tahadhari mapema kabisa mabosi wa Anfield kwamba wote, Mane na Salah watachungulia mlango wa kutokea kama itawekwa mezani mkwanja mrefu hasa ukizingatia kwamba soka lenyewe la kisasa limekuwa la maslahi zaidi.

Alisema: “Kila klabu inauza katika dunia ya sasa. Ona klabu kama Barcelona ililazimika kumuuza Neymar.

“Kinachovutia soka kwa sasa ni mishahara wanayokwenda kupata wachezaji. Mchezaji yeyote, awe Sadio Mane au Mo Salah, yeyoye hapo akipewa ofa ya mamilioni ya Pauni kwa wiki na klabu yoyote, atakwenda kuungana nayo bila ya kujali ubora wala msimamo. Hivyo ndivyo soka la sasa lilivyo.

“Tumeshuhudia wachezaji wengi sana mahiri wakiondoka Liverpool - Fernando Torres, Luis Suarez, Philippe Coutinho. Ni jambo zuri kwamba Liverpool kwa sasa bado wana wachezaji wenye nguvu ndani ya uwanja, lakini ni wazi wachezaji wazuri wanakuja na kuondoka.

“Siku zote nimekuwa nikiwaambia mashabiki washangilie klabu sio wachezaji. Mchezaji hawezi kulazimishwa kubaki kwenye klabu bila ya matakwa yake, kwa sababu anajiona ana nguvu.”