Mkomola aiona neema Arsenal Kyiv ya Ukraine

MSHAMBULIAJI mpya wa Arsenal Kyiv, Yohana Mkomola anaamini kujiunga kwake na chama hilo linaloshiriki Ligi Kuu Ukraine ni mwanzo wa safari yake kutaka kucheza ligi za mataifa makubwa zaidi kisoka barani Ulaya.

Mkomola alijiunga na Arsenal Kyiv kwa kusaini mkataba wa miaka mitatu baada ya kufuzu majaribio ambayo alienda kuyafanya akiwa na beki kinda wa Mtibwa Sugar, Nickson Kibabage.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, alisema alikuwa na shauku ya kucheza Ulaya na kupata kwake nafasi ya kujiunga na Arsenal Kyiv ni kama mwanzo wa safari yake ya kupigania ndoto zake.

“Mara kadhaa nilikuwa nikizungumza na marafiki zangu kuwa ipo siku nitacheza soka Ulaya, wapo ambao walikuwa wakinicheka na pale an mambo yalikuwa hayaendi waliona ni kama ndio nimepotea vile.

“Nashukuru Mungu hatimaye nimepata fursa ambayo natakiwa kuitumia ili nipige hatua, sina mawazo kuwa hapa ndio nimefika, najitahidi kuzoea mazingira ili iwe rahisi kuonyesha uwezo wangu.

“Nimepata mapokezi mazuri ambayo sikuyategemea. Sina papara za kutaka kuanza kucheza, kocha akiona muda sahihi umefika nadhani ataanza kunitumia,” alisema kinda huyo.

Mkomola ni miongoni kwa wachezaji waliowahi kuichezea Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, katika mashindano ya Afcon yaliyofanyika Gabon mwaka 2017.

Kabla ya kwenda Arsenal Kiev, Mkomola aliyekuwa akiichezea African Lyon, aliwahi kufanya majaribio na kufaulu katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, lakini umri ukatibua dili.

Mkomola alisema Tunisia alikuwa na umri wa miaka chini ya 18, hivyo Etoile ilimrudisha Tanzania ili akue kabla ya kumchukua, ndipo Yanga ikamsajili, lakini akakosa namba na kukimbilia Lyon.